Acts 26

Paulo Ajitetea Mbele Ya Agripa

1Ndipo Agripa akamwambia Paulo, “Unayo ruhusa kujitetea.”

Hivyo Paulo akawaashiria kwa mkono wake, akaanza kujitetea, akasema:
2“Mfalme Agripa, najiona kuwa na heri kusimama mbele yako leo ninapojitetea kuhusu mashtaka yote ya Wayahudi, 3hasa kwa sababu unajua vyema desturi zote za Kiyahudi na ya kuwa wewe unajua kwa undani mila na masuala ya mabishano. Kwa hiyo, nakusihi unisikilize kwa uvumilivu.

4“Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu. 5Wao wamefahamu kwa muda mrefu na wanaweza kushuhudia kama wakipenda, kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu niliishi nikiwa Farisayo. 6Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo. 7Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii mchana na usiku. 8Kwa nini ye yote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu?

9“Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Yesu wa Nazareti. 10Nami hayo ndiyo nilivyofanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwatia wengi wa watakatifu gerezani na walipokuwa wakiuawa, nilipiga kura yangu kuunga mkono. 11Mara nyingi nilikwenda kutoka sinagogi moja hadi jingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilikwenda miji ya kigeni ili kuwatesa.

Paulo Aeleza Kuhusu Kuongoka Kwake

12“Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninakwenda Dameski, nilikuwa na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani. 13Ilikuwa yapata adhuhuri, Ee Mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni kali kuliko jua, iking'aa kunizunguka pande zote mimi na wale niliokuwa pamoja nao. 14Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’

15“Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’

“Naye Bwana akajibu, ‘Ni Mimi Yesu unayenitesa.
16Lakini sasa inuka usimame kwa miguu yako, kwa sababu nimekutokea kwa kusudi hili, ili kukuweka utumike na kushuhudia juu ya mambo ambayo umeyaona na yale nitakayokutokea kwayo. 17Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu Mataifa ambao ninakutuma kwao, 18uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni na kutoka kwenye nguvu za Shetani, wamgeukie Mungu ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’

19“Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni, 20bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Uyahudi na pia kwa watu Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao. 21Ni kwa sababu hii Wayahudi walinikamata nilipokuwa Hekaluni, wakataka kuniua. 22Hadi leo nimepata msaada kutoka kwa Mungu na hivyo nasimama hapa nikishuhudia wakubwa na wadogo, bila kusema cho chote zaidi ya yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia: 23kwamba Kristo
26:23 Yaani Masiya
atateswa na kwamba yeye atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, atatangaza nuru kwa watu wake na kwa watu Mataifa.”

Paulo Aeleza Juu Ya Kuhubiri Kwake

24Paulo alipokuwa akifanya utetezi huu, Festo akasema kwa sauti kubwa, “Paulo, wewe umerukwa na akili! Kusoma kwingi kunakufanya uwe kichaa!”

25Lakini Paulo akajibu, “Mimi sijarukwa na akili, mtukufu sana Festo, bali nanena kweli nikiwa na akili zangu timamu. 26Naam, Mfalme anajua kuhusu mambo haya yote, nami nasema naye kwa uhuru. Kwa sababu nina hakika kwamba hakuna hata mojawapo ya mambo haya asilolijua, kwa kuwa hayakufanyika mafichoni. 27Mfalme Agripa, je, unaamini manabii? Najua kuwa unaamini.”

28Agripa akamwambia Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe Mkristo?”

29Paulo akasema, “Ikiwa ni kwa haraka au la, namwomba Mungu, si wewe peke yako bali pia wale wote wanaonisikiliza leo, wawe kama mimi nilivyo, isipokuwa minyororo hii.”

30Baada ya kusema hayo, mfalme akainuka pamoja na mtawala na Bernike na wale waliokuwa wameketi pamoja nao. 31Wakati walipokuwa wakiondoka, wakaambiana “Mtu huyu hafanyi jambo lo lote linalostahili kufa au kufungwa.”

32Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kuachwa huru kama hangekuwa amekata rufaa kwa Kaisari.”

Copyright information for Neno