Colossians 1

Salamu

Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu na Timotheo ndugu yetu:

Kwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Kristo, waishio Kolosai:

Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu.

Shukrani Na Maombi

Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunapowaombea ninyi, kwa sababu tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na juu ya upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote, imani na upendo ule utokao katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani, ile Injili iliyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote. Mlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, yeye aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu, ambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho.

Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatukukoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana na mpate kumpendeza kwa kila namna: Mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikuwa katika kumjua Bwana. 11 Mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu, nanyi kwa furaha 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi kwa njia ya damu yake.

Ukuu Wa Kristo

15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwa yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa, vile vitu vinavyoonekana na vile visivyoonekana, kama ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala, vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwapo kabla ya vitu vyote na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani, Kanisa, naye ni wa mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba ukamilifu wake wote wa Kiungu uwe ndani yake 20 na kwa njia ya Mwanawe aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, ikiwa ni vitu vilivyoko duniani au vilivyoko mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake iliyomwagika msalabani.

21 Hapo kwanza ninyi mlikuwa mmetengana na Mungu na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mwenendo wenu mbaya. 22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Kristo kwa kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama, 23 mradi tu kwamba mnaendelea kuwa waaminifu, mkiwa mmefanywa imara na thabiti katika imani, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa na Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu na ambayo mimi Paulo, nimekuwa mtumwa wake.

Taabu Ya Paulo Kwa Ajili Ya Kanisa

24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni Kanisa. 25 Mimi nimekuwa mtumishi wa Kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu. 26 Siri hii ilikuwa imefichika kwa karne nyingi na vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. 27 Kwao, Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.

28 Yeye Kristo ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo. 29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zile ambazo kwa uweza mwingi hutenda kazi ndani yangu.

Copyright information for Neno