Colossians 2

1Kwa kuwa nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia na kwa ajili ya wote wale ambao hawajapata kuniona mimi binafsi. 2Kusudi langu ni kuwa watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu kikamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe, 3ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa. 4Nawaambia mambo haya ili mtu ye yote asiwadanganye kwa maneno ya kuwashawishi. 5Kwa maana ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, lakini niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi gani uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo.

Ukamilifu Wa Maisha Katika Kristo

6Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, 7mwe na mizizi, mkiwa mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa na kufurika kwa wingi wa shukrani.

8Angalieni mtu ye yote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu ambayo siyo ya Kristo.

9Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye yeye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka. 11Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, 12mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu.

13Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili pamoja na amri zake, aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. 15Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba wa Kristo.

16Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au Siku ya Sabato. 17Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo. 18Mtu ye yote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kumnyenyekea yeye na kuabudu malaika, akidumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu, 19wala hakishiki kwa uthabiti kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, ambao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.

Maonyo Dhidi Ya Walimu Wa Uongo

20Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama vile ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri: 21“Msishike! Msionje! Msiguse!”? 22Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu huo msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. 23Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

Copyright information for Neno