Daniel 1

Mafunzo Ya Danieli Huko Babeli

1Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi. 2Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza pamoja na baadhi ya vyombo kutoka katika Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari naye akaviweka katika nyumba ya hazina ya mungu wake.

3Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa jumba lake la kifalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya kifalme na kutoka watu mashuhuri, 4vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha ujuzi katika kila elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo. 5Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka katika meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.

6Miongoni mwa hawa vijana baadhi walikuwa kutoka Yuda: Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. 7Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya, Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki na Azaria akamwita Abednego.

8Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha kifalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa kwa ajili ya kutokujinajisi kwa njia hii. 9Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonyesha upendeleo na huruma kwa Danieli, 10lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu ni mbaya kuliko za vijana rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”

11Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, 12“Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe cho chote ila nafaka na mboga za majani
1.12 Nafaka na mboga za majani yaani zeroimu kwa Kiebrania ina maana ya ngano, shayiri, jamii ya kunde-maharagwe, kunde, choroko, n.k.
tule na maji ya kunywa.
13Ndipo ulinganishe kuonekana kwetu na vijana wanaokula chakula cha kifalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.” 14Basi akakubali jambo hili akawajaribu kwa siku kumi.

15Mwisho wa zile siku kumi walionekana kuwa na afya na kunawiri zaidi kuliko ye yote kati ya wale vijana waliokula chakula cha kifalme. 16Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.

17Mungu akawapa hawa vijana waume wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.

18Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza. 19Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyekuwa amelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme. 20Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwaona bora mara kumi zaidi kuliko waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.

21Naye Danieli akabaki huko mpaka mwaka wa kwanza wa kutawala kwake Mfalme Koreshi.

Copyright information for Neno