Deuteronomy 20

Kwenda Vitani

Mtakapokwenda vitani kupigana na adui zenu na mkaona farasi na magari ya vita na jeshi kubwa kuliko lenu, msiwaogope, kwa sababu BWANA Mungu wenu aliyewatoa kutoka Misri, atakuwa pamoja nanyi. Wakati mtakapokaribia kwenda vitani, kuhani atakuja mbele na kuhutubia jeshi. Atasema: “Sikia, Ee Israeli, leo unakwenda vitani kupigana na adui zako. Usife moyo wala usiogope, usitishwe wala usitiwe hofu mbele yao. Kwa kuwa BWANA Mungu wenu ndiye huenda pamoja nanyi kuwapigania dhidi ya adui zenu na kuwapatia ushindi.”

Maafisa wataliambia jeshi: “Je, kuna ye yote aliyejenga nyumba mpya ambayo haijawekwa wakfu? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akaiweka wakfu. Je, kuna ye yote aliyepanda shamba la mizabibu na hajaanza kulifurahia? Yeye na arudi nyumbani, au sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akalifurahia. Je, kuna ye yote aliyeposa mwanamke na hajamwoa? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akamwoa.” Kisha maafisa wataongeza haya, “Je, kuna mtu anayeogopa ama kufa moyo? Yeye na arudi nyumbani ili ndugu zake nao wasije wakafa moyo pia.” Wakati maafisa watakapomaliza kuzungumza na jeshi, watawateua wakuu wa vikosi.

10 Wakati mtakapokwenda kushambulia mji, wapeni watu wake masharti ya amani. 11 Wakikubali na kuwafungulia malango yao, watu wake wote watawatumikia kwa kufanya kazi ngumu na watawatumikia. 12 Ikiwa watakataa kufanya mapatano ya amani na wakiwaingiza katika vita, basi mtauzunguka mji huo kwa vita. 13 Wakati BWANA Mungu wenu atakapouweka mji huo mkononi mwenu, waueni kwa upanga wanaume wote waliomo ndani yake. 14 Kwa upande wa wanawake, watoto, mifugo na kila kitu kingine cho chote ndani ya huo mji, mnaweza kuvichukua kama nyara kwa ajili yenu. Nanyi mnaweza kuzitumia hizo nyara ambazo BWANA Mungu wenu amewapa kutoka kwa adui zenu. 15 Hivi ndivyo mtakavyofanya kwa miji yote ambayo iko mbali nanyi, ambayo haimilikiwi na mataifa ya karibu.

16 Hata hivyo, katika miji ya mataifa ambayo BWANA Mungu wenu anawapa kama urithi, msiache kitu cho chote hai kinachopumua. 17 Waangamizeni kabisa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, kama BWANA Mungu wenu alivyowaamuru. 18 La sivyo, watawafundisha kufuata mambo yote ya machukizo wanayofanya wakiabudu miungu yao, nanyi mtatenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wenu.

19 Wakati mtakapouzunguka mji kwa vita kwa muda mrefu, mkipigana dhidi yake ili kuuteka, msiharibu miti yake kwa kuikata kwa shoka, kwa sababu mtaweza kula matunda yake. Hivyo msiikate. Je, miti hiyo ya mashambani ni watu, hata muizingire? 20 Hata hivyo, mnaweza kuikata miti ambayo sio miti ya matunda na kuitumia kujenga ngome, mpaka mji ulio katika vita na ninyi utakapoanguka.

Copyright information for Neno