Esther 6

Mordekai Anapewa Heshima

Usiku ule mfalme hakupata usingizi, hivyo akaagiza aletewe kitabu cha kumbukumbu za matukio ya utawala wake, asomewe. Kitabu hicho kilikutwa na kumbukumbu kwamba Mordekai alikuwa amefichua jinsi Bigthana na Tereshi, waliokuwa maafisa wawili wa mfalme, walinzi wa lango walivyokuwa wamepanga hila ya kumwua Mfalme Ahusuero.

Mfalme akauliza, “Je, ni heshima na shukrani gani Mordekai alipokea kwa ajili ya jambo hili?”

Watumishi wake wakajibu, “Hakuna lo lote alilofanyiwa.”

Mfalme akasema, “Ni nani yuko uani?” Wakati uo huo Hamani alikuwa ameingia ua wa nje wa jumba la mfalme kusema na mfalme kuhusu kumwangika Mordekai katika mahali pa kuangikia watu alipokuwa amepajenga kwa ajili yake.

Watumishi wake wakamjibu, “Hamani amesimama uani.”

Mfalme akaamuru, “Mleteni ndani.”

Hamani alipoingia, mfalme alimwuliza, “Afanyiwe nini mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu?”

Basi Hamani akawaza moyoni mwake, “Ni nani mwingine ambaye mfalme angemheshimu kuliko mimi?”
Kwa hiyo akamjibu mfalme, “Kwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu, aletewe joho la kifalme ambalo mfalme ameshalivaa na farasi ambaye mfalme alishampanda, ambaye amevikwa taji ya kifalme kichwani mwake. Kisha joho na farasi vikabidhiwe kwa mmojawapo wa wakuu wa mfalme anayeheshimika sana. Nao wamvike mtu yule ambaye mfalme anapenda kumheshimu, na aongozwe akiwa juu ya farasi kupitia barabara za mji, wakitangaza mbele yake, ‘Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu!’ ”

10 Mfalme akamwamuru Hamani, “Nenda mara moja, chukua joho na farasi na ufanye kama vile ulivyopendekeza kwa Mordekai Myahudi, akaaye langoni mwa mfalme. Usipuuze kufanya kitu cho chote ulichoshauri.”

11 Hivyo Hamani akachukua joho na farasi.

Akamvika Mordekai, na kumpandisha juu ya farasi akamtembeza katika barabara za mji akitangaza mbele yake, “Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme anapenda kumheshimu!”

12 Baadaye Mordekai akarudi kwenye lango la mfalme. Lakini Hamani akakimbia nyumbani, akiwa amejaa huzuni, 13 naye akamweleza Zereshi mkewe pamoja na rafiki zake wote kila kitu ambacho kimempata.

Washauri wake pamoja na Zereshi mkewe wakamwambia, “Kwa kuwa Mordekai, ambaye mbele yake umeanza kuanguka ni wa asili ya Kiyahudi, huwezi kushindana naye, kwa hakika utaanguka!”
14 Walipokuwa bado wakizungumza naye, matowashi wa mfalme wakaja na kumharakisha Hamani aende katika karamu aliyoiandaa Esta.

Copyright information for Neno