Ezra 3

Madhabahu Yajengwa Tena

1 aMwezi wa saba ulipowadia baada ya Waisraeli kukaa katika miji yao, watu wote walikusanyika huko Yerusalemu kama mtu mmoja. 2 bYeshua mwana wa Yosadaki na makuhani wenzake, Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na wenzake walianza kujenga madhabahu ya Mungu wa Israeli ili kumtolea dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto juu yake, kulingana na ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu. 3 cIngawa waliwaogopa watu waliowazunguka, walijenga madhabahu juu ya ule msingi wake, wakamtolea Bwana dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto juu yake za asubuhi na za jioni. 4 dKisha kulingana na kile kilichoandikwa, wakaiadhimisha Sikukuu ya Vibanda wakitoa idadi ya sadaka za kuteketezwa kama ilivyohitajika kila siku sawasawa na ilivyoagizwa. 5 eBaada ya hayo, walitoa sadaka za kuteketezwa za kawaida, sadaka za Mwezi Mwandamo na dhabihu zote za sikukuu takatifu za Bwana zilizoamriwa, pamoja na zile sadaka za hiari zilizotolewa kwa Bwana. 6Ingawa bado msingi wa Hekalu la Bwana ulikuwa haujawekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Bwana tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.

Kujenga Upya Hekalu

7 fKisha watu wakawapa mafundi wa uashi na useremala fedha, wakawapa watu wa Sidoni na Tiro vyakula, vinywaji na mafuta ili waweze kuleta magogo ya mierezi kwa njia ya bahari kutoka Lebanoni hadi Yafa, kama alivyoagiza Koreshi mfalme wa Uajemi.

8 gKatika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri kuanzia miaka ishirini au zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya Bwana. 9 hYeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu.

10 i jWajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Bwana, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumtukuza Bwana, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. 11 kWaliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Bwana hivi:

“Yeye ni mwema;
upendo wake kwa Israeli
wadumu milele.”
Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Bwana, kwa sababu msingi wa nyumba ya Bwana ulikuwa umewekwa.
12 lLakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha. 13 mHakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.

Copyright information for SwhNEN