Galatians 3

Imani Au Kushika Sheria?

1Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaloga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulibiwa. 2Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

6Kama vile Abrahamu, alivyomwamini Mungu ikahesabiwa kwake kuwa haki. 7Fahamuni basi kwamba wale walio na imani hao ndio watoto wa Abrahamu. 8Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” 9Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.

Sheria Na Laana

10Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria, wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Amelaaniwa mtu yule asiyeshika na kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” 11Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu ye yote anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” 12Lakini sheria haitegemei imani, kinyume chake, “Ye yote atendaye matendo ya sheria ataishi kwa sheria.” 13Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” 14Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.

Sheria Na Ahadi

15Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka katika maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. 16Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. 17Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kulibatilisha. 18Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi.

Kusudi La Sheria

19Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamuriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.

21Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. 22Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini.

23Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. 24Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. 25Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.

Watoto Wa Mungu

26Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

Copyright information for Neno