Genesis 16

Hagari Na Ishmaeli

1 aBasi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mtumishi wa kike Mmisri jina lake Hagari, 2 bhivyo Sarai akamwambia Abramu, “Bwana amenizuilia kupata watoto. Nenda, ukakutane kimwili na mtumishi wangu wa kike, huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.”

Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema.
3 cHivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mtumishi wake wa kike wa Kimisri, Hagari na kumpa mumewe awe mke wake. 4 dAkakutana kimwili na Hagari, naye akapata mimba.

Hagari alipojua kuwa ana mimba, alianza kumdharau Sarai.
5 eNdipo Sarai akamwambia Abramu, “Unawajibika na manyanyaso ninayoyapata. Nilimweka mtumishi wangu mikononi mwako, sasa kwa vile anajua kwamba ana mimba, ananidharau mimi. Bwana na aamue kati yako na mimi.”

6 fAbramu akamwambia, “Mtumishi wako yuko mikononi mwako. Mtendee lolote unalofikiri ni bora zaidi.” Ndipo Sarai akamtesa Hagari, hivyo akamtoroka.

7 gMalaika wa Bwana akamkuta Hagari karibu na chemchemi huko jangwani; ilikuwa chemchemi ile iliyokuwa kando ya barabara iendayo Shuri. 8 hMalaika akamwambia, “Hagari, mtumishi wa Sarai, umetokea wapi, na unakwenda wapi?”

Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.”

9Ndipo malaika wa Bwana akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.” 10 iMalaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.”

11 jPia malaika wa Bwana akamwambia:

“Wewe sasa una mimba
nawe utamzaa mwana.
Utamwita jina lake Ishmaeli,
Ishmaeli maana yake Mungu husikia.

kwa sababu Bwana amesikia juu ya huzuni yako.
12 lAtakuwa punda-mwitu katikati ya wanadamu,
mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu
na mkono wa kila mtu dhidi yake,
naye ataishi kwa uhasama
na ndugu zake wote.”
13 mHagari akampa Bwana aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.” 14 nNdiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi,
Beer-Lahai-Roi maana yake Yeye Aliye Hai Anionaye Mimi.
ambacho bado kipo huko hata leo kati ya Kadeshi na Beredi.

15 pHivyo Hagari akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hagari aliyemzalia, Ishmaeli. 16 qAbramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita wakati Hagari alipomzalia Ishmaeli.

Copyright information for SwhNEN