Genesis 18

Wageni Watatu

1 a Bwana akamtokea Abrahamu karibu na mialoni ya Mamre wakati alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri. 2 bAbrahamu akainua macho akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, aliharakisha kutoka kwenye ingilio la hema lake kuwalaki na kuwasujudia hadi nchi.

3Akasema, “Kama nimepata kibali machoni penu, ee bwana wangu, usimpite mtumishi wako. 4 cAcha yaletwe maji kidogo, kisha ninyi nyote mnawe miguu yenu na mpumzike chini ya mti huu. 5 dNiruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.”

Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.”

6 eHivyo Abrahamu akaharakisha akaingia hemani kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”

7 fKisha Abrahamu akakimbia kwenda kwenye kundi, akachagua ndama mzuri, laini na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha. 8 gKisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.

9 hWakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?”

Akasema, “Yuko huko, ndani ya hema.”

10 iKisha Bwana akasema, “Hakika nitakurudia tena majira kama haya mwakani na Sara mkeo atakuwa ana mwana.”

Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema, lililokuwa nyuma yake.
11 jAbrahamu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12 kHivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”

13 lNdipo Bwana akamwambia Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ 14 mJe, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa Bwana? Nitakurudia mwakani majira kama haya, naye Sara atakuwa na mwana.”

15Sara akaogopa kwa kuwa alidanganya na kusema, “Mimi sikucheka.”

Lakini Bwana akasema, “Ndiyo, ulicheka!”

Abrahamu Aiombea Sodoma

16Wakati watu hao waliposimama ili waondoke, walielekeza nyuso zao Sodoma, Abrahamu akawatoa kitambo kidogo ili awasindikize. 17 nNdipo Bwana akasema, “Je, nimfiche Abrahamu jambo ninalokusudia kufanya? 18 oHakika Abrahamu atakuwa taifa kubwa na lenye nguvu, kupitia kwake mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. 19 pKwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya Bwana, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili Bwana atimize ahadi yake kwa Abrahamu.”

20 qBasi Bwana akasema, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi yao inasikitisha sana, 21 rkwamba nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.”

22 sBasi wale watu wakageuka wakaenda kuelekea Sodoma, lakini Abrahamu akabaki amesimama mbele za Bwana. 23 tNdipo Abrahamu akamsogelea akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? 24 uJe, ikiwa watakuwepo watu wenye haki hamsini katika mji huo, hivi kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo ndani yake? 25 vHilo na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo, kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Iwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya lililo sawa?”

26 Bwana akasema, “Kama nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitausamehe huo mji wote kwa ajili yao.”

27 wKisha Abrahamu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu; 28je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?”

Bwana akamwambia, “Kama nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.”

29Abrahamu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?”

Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.”

30 xNdipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?”

Akajibu, “Sitapaangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.”

31Abrahamu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, kama wakipatikana huko watu ishirini tu?”

Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”

32 yAbrahamu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?”

Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.”

33 z Bwana alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, akaondoka, naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake.

Copyright information for SwhNEN