Genesis 3

Kuanguka Kwa Mwanadamu

1 aBasi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

2 bMwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

4 cLakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 dKwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

6 eMwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala. 7 fNdipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika.

8 gNdipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya Bwana Mungu alipokuwa akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka mbele za Bwana Mungu katikati ya miti ya bustani. 9 hLakini Bwana Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?”

10 iNaye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.”

11 jMungu akamuuliza, “Ni nani aliyekuambia ya kuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?”

12 kAdamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.”

13 lNdipo Bwana Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

14 mHivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,

“Umelaaniwa kuliko wanyama wote
wa kufugwa na wa porini!
Utatambaa kwa tumbo lako
na kula mavumbi
siku zote za maisha yako.
15 nNami nitaweka uadui
kati yako na huyo mwanamke,
na kati ya uzao wako na wake,
yeye atakuponda kichwa,
nawe utamuuma kisigino.”
16 oKwa mwanamke akasema,

“Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;
kwa utungu utazaa watoto.
Tamaa yako itakuwa kwa mumeo
naye atakutawala.”
17 pKwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

“Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,
kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo
siku zote za maisha yako.
18 qItazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,
nawe utakula mimea ya shambani.
19 rKwa jasho la uso wako
utakula chakula chako
hadi utakaporudi ardhini,
kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,
kwa kuwa wewe u mavumbi
na mavumbini wewe utarudi.”
20 sAdamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.

21 Bwana Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. 22 tKisha Bwana Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyoosha mkono wake na kuchuma pia kutoka mti wa uzima akala, naye akaishi milele.” 23 uHivyo Bwana Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa. 24 vBaada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki ya Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika huku na huko kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.

Copyright information for SwhNEN