Genesis 41

Ndoto Za Farao

Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto: Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Nile, wakati ng'ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye manyasi. Baada yao ng'ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea mtoni Nile wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto. Wale ng'ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka.

Farao akaingia usingizini tena akaota ndoto ya pili: Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja. Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyonyaushwa na upepo wa mashariki. Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, kumbe ilikuwa ndoto.

Asubuhi yake, alifadhaika akilini, hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.

Ndipo mnyweshaji mkuu alipomwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kuhusu kosa langu. 10 Wakati fulani Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa ulinzi. 11 Kila mmoja wetu aliota ndoto katika usiku mmoja na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. 12 Basi kijana wa Kiebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, alikuwa mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupa kila mtu tafsiri ya ndoto yake. 13 Nayo mambo yakawa sawa kabisa na jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu na huyo mtu mwingine akaangikwa.”

14 Basi, Farao akatuma Yosefu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake akaenda mbele ya Farao.

15 Farao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.”

16 Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”

17 Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Nile, 18 nikawaona ng'ombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni wakaja kujilisha kwenye manyasi. 19 Baada ya hao, ng'ombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ng'ombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri. 20 Hao ng'ombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ng'ombe saba walionona waliojitokeza kwanza. 21 Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini.

22 “Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja. 23 Baada ya hayo masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki. 24 Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna ye yote aliyeweza kunifasiria.”

25 Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto iyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 26 Ng'ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba, ni ndoto iyo hiyo moja. 27 Ng'ombe saba waliokonda na wabaya wale waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki, ni miaka saba ya njaa.

28 “Ni kama vile nilivyomwambia Farao: Mungu amemwonyesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 29 Miaka saba ya neema inakuja katika nchi yote ya Misri, 30 lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo neema yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.

31 “Neema iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. 32 Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.

33 “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. 34 Farao na aweke wenye amri nchini kote wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya neema. 35 Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. 36 Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”

37 Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote. 38 Hivyo Farao akawauliza, “Je tunaweza kumpata ye yote kama mtu huyu, ambaye Roho wa Mungu yumo ndani yake?”

39 Ndipo Farao akamwambia Yosefu, “Maadamu Mungu amekufunulia yote haya, hakuna mwingine ye yote mwenye akili na hekima kama wewe. 40 Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

Yosefu Msimamizi Wa Misri

41 Kwa hiyo Farao akamwambia Yosefu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.” 42 Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yosefu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43 Akampandisha katika gari lake la farasi kama msaidizi wake, watu wakatangulia wakishangilia, wakisema, “Achieni njia!” Ndivyo Farao alivyomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.

44 Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.” 45 Farao akamwita Yosefu Safenath-Panea, pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni
41:45 Yaani Heliopoli (Mji wa Jua)
, kuwa mke wake. Ndipo Yosefu akaitembelea nchi yote ya Misri.

46 Yosefu alikuwa na miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao mfalme wa Misri. Naye Yosefu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri. 47 Katika ile miaka saba ya neema nchi ilizaa mazao kwa wingi sana. 48 Yosefu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya neema nchini Misri, akakihifadhi katika ghala za miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo. 49 Yosefu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari, ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi sana kupita kipimo.

50 Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alikuwa amemzalia Yosefu wana wawili wa kiume. 51 Yosefu akamwita mzaliwa wake wa kwanza Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.” 52 Mwana wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.”

53 Ile miaka saba ya neema huko Misri ikaisha, 54 nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yosefu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula. 55 Wakati nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao alipowaagiza Wamisri wote, akisema, “Nendeni kwa Yosefu, nanyi mfanye anachowaambia.”

56 Wakati njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yosefu akafungua ghala za vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri. 57 Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yosefu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.

Copyright information for Neno