Genesis 6

Sababu Za Gharika

Watu walipoanza kuongezeka idadi katika uso wa dunia na watoto wa kike wakazaliwa kwao, wana wa Mungu wakawaona kuwa hao binti za wanadamu walikuwa wazuri wa sura, wakaoa ye yote miongoni mwao waliyemchagua. Ndipo BWANA akasema, “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa, siku zake zitakuwa miaka 120.”

Wanefili walikuwako duniani siku hizo, na baadaye, hao wana wa Mungu walipoingia kwa hao binti za wanadamu na kuzaa nao. Wanefili walikuwa mashujaa na watu waliojulikana wa zamani hizo.

BWANA akaona jinsi ambavyo uovu wa mwanadamu umekuwa mkubwa duniani na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. BWANA akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. Kwa hiyo BWANA akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kwa kuwaumba.” Lakini Noa akapata kibali machoni pa BWANA.Hivi ndivyo vizazi vya Noa.Noa alikuwa mtu wa haki, asiye na lawama miongoni mwa watu wa wakati wake, tena alitembea na Mungu.
10 Noa alikuwa na wana watatu: Shemu, Hamu na Yafethi.

11 Wakati huu dunia ilikuwa imejaa uharibifu na jeuri machoni pa Mungu. 12 Mungu akaona jinsi dunia ilivyoharibika, kwa maana watu wote duniani walikuwa wameharibu njia zao. 13 Kwa hiyo Mungu akamwambia Noa, “Nitawaangamiza watu wote, kwa kuwa dunia imejaa jeuri kwa sababu yao. Hakika mimi nitaangamiza watu pamoja na dunia. 14 Kwa hiyo jitengenezee safina kubwa kwa mbao za mvinje, tengeneza vyumba ndani yake na uipake lami ndani na nje. 15 Hivi ndivyo utakavyoitengeneza: Safina iwe na urefu wa dhiraa 300
6.15Dhiraa 300 ni sawa na mita 135
, upana wake dhiraa hamsini
6.15Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5
, na kimo chake dhiraa thelathini
6.15Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5
.
16 Itengenezee paa na umalizie safina kwa kuacha nafasi ya dhiraa moja
6.16Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45
juu. Weka mlango ubavuni mwa safina, na uifanye ya ghorofa ya chini, ya kati na ya juu.
17 Nitaleta gharika ya maji juu ya nchi ili kuangamiza uhai wote chini ya mbingu, kila kiumbe chenye pumzi ya uhai ndani yake. Kila kitu juu ya nchi kitaangamia. 18 Lakini Mimi nitaweka Agano langu na wewe, nawe utaingia ndani ya Safina, wewe pamoja na mke wako, wanao na wake zao. 19 Utaingiza ndani ya Safina kila aina ya kiumbe hai wawili wawili, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja na wewe. 20 Wawili wa kila aina ya ndege, wa kila aina ya mnyama na wa kila aina ya kitambaacho ardhini watakuja kwako ili wahifadhiwe hai. 21 Utachukua kila aina ya chakula kitakacholiwa, na ukiweke akiba kama chakula kwa ajili yako na yao.”

22 Noa akafanya kila kitu sawasawa kama vile Mungu alivyomwamuru.

Copyright information for Neno