Genesis 9

Mungu Aweka Agano Na Noa

1Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia. 2Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.

4“Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. 5Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake. 6“Ye yote amwagaye damu ya mwanadamu,
damu yake itamwagwa na mwanadamu,
kwa kuwa katika mfano wa Mungu,
Mungu alimuumba mwanadamu.


7Kuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.”

8Ndipo Mungu akamwambia Noa na wanawe pamoja naye: 9“Sasa mimi ninaweka Agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, 10pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wote wa porini, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi, kila kiumbe hai duniani. 11Ninaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.”

12Mungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo: 13Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia. 14Wakati wo wote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni, 15nitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. 16Wakati wo wote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”

17Hivyo Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya Agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”

Wana Wa Noa

18Wana wa Noa waliotoka ndani ya safina ni: Shemu, Hamu na Yafethi. (Hamu ndiye aliyekuwa baba wa Kanaani.) 19Hawa ndio waliokuwa wana watatu wa Noa, kutokana nao watu walienea katika dunia.

20Noa akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu. 21Alipokunywa huo mvinyo wake akalewa na akalala uchi kwenye hema lake. 22Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.

24Noa alipolevuka kutoka kwenye mvinyo wake na kujua lile ambalo mwanawe mdogo kuliko wote alilokuwa amemtendea, 25akasema, “Alaaniwe Kanaani!
Atakuwa mtumwa wa chini sana
kuliko watumwa wote kwa ndugu zake.”26Pia akasema, “Abarikiwe BWANA, Mungu wa Shemu!
Kanaani na awe mtumwa wa Shemu.
27Mungu na apanue mipaka ya Yafethi;
Yafethi na aishi katika mahema ya Shemu,
na Kanaani na awe mtumwa wake.”28Baada ya gharika Noa aliishi miaka 350. 29Noa alikuwa na jumla ya miaka 950, ndipo akafa.

Copyright information for Neno