Hebrews 5

1Kwa maana kila Kuhani Mkuu anayechaguliwa miongoni mwa wanadamu anawekwa kuwawakilisha kwa mambo yanayomhusu Mungu, ili apate kutoa matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi. 2Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka. 3Hii ndiyo sababu inampasa kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe na vivyo hivyo kwa ajili ya dhambi za watu. 4Hakuna anayejitwalia heshima hii mwenyewe, ni lazima aitwe na Mungu, kama vile Aroni alivyoitwa. 5Pia Kristo hakujitwalia utukufu yeye mwenyewe wa kuwa Kuhani Mkuu, bali Mungu alimwambia, “Wewe ni Mwanangu,
mimi leo nimekuzaa.”6Pia mahali pengine asema, “Wewe ndiwe kuhani milele,
kwa mfano wa Melkizedeki.”7Katika siku za maisha ya Yesu hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu. 8Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utii kutokana na mateso aliyoyapata, 9akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii, 10naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.

Wito Wa Kukua Kiroho

11Tunayo mengi ya kusema kuhusu habari ya ukuhani huu, lakini ni vigumu kuyaeleza, kwa sababu ninyi ni wazito wa kuelewa. 12Kwa hakika, ingawa mpaka wakati huu ingewapasa kuwa walimu, lakini bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya Neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu! 13Kwa maana ye yote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki. 14Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.

Copyright information for Neno