Hosea 13

Hasira Ya Bwana Dhidi Ya Israeli

1 aWakati Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka,
alikuwa ametukuzwa katika Israeli.
Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali
naye akafa.
2 bSasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi;
wanajitengenezea sanamu
kutokana na fedha yao,
vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari,
vyote kazi ya fundi stadi.
Inasemekana kuhusu hawa watu,
“Hutoa dhabihu za binadamu
na kubusu sanamu za ndama.”
3 c dKwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi,
kama umande wa alfajiri utowekao,
kama makapi yapeperushwayo
kutoka sakafu ya kupuria nafaka,
kama moshi utorokao kupitia dirishani.

4 e“Bali mimi ndimi Bwana Mungu wenu,
niliyewaleta ninyi toka Misri.
Msimkubali Mungu mwingine ila mimi,
hakuna Mwokozi isipokuwa mimi.
5 fNiliwatunza huko jangwani,
katika nchi yenye joto liunguzalo.
6 gNilipowalisha, walishiba,
waliposhiba, wakajivuna,
kisha wakanisahau mimi.
7 hKwa hiyo nitakuja juu yao kama simba,
kama chui nitawavizia kando ya njia.
8 iKama dubu aliyenyangʼanywa watoto wake,
nitawashambulia na kurarua vifua vyenu.
Kama simba nitawala;
mnyama pori atawararua vipande vipande.

9 j“Ee Israeli, umeangamizwa,
kwa sababu wewe u kinyume nami,
kinyume na msaidizi wako.
10 kYuko wapi mfalme wako,
ili apate kukuokoa?
Wako wapi watawala wako katika miji yako yote
ambao ulisema kuwahusu,
‘Nipe mfalme na wakuu’?
11 lHivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme
na katika ghadhabu yangu nilimwondoa.
12 mKosa la Efraimu limehifadhiwa,
dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu.
13 nUtungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia,
lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima;
wakati utakapowadia hatatoka
katika tumbo la mama yake.

14 o“Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi,
nitawakomboa kutoka mautini.
Yako wapi, ee mauti, mateso yako?
Uko wapi, ee kuzimu, uharibifu wako?

“Sitakuwa na huruma,
15 phata ingawa Efraimu atastawi
miongoni mwa ndugu zake.
Upepo wa mashariki kutoka kwa Bwana utakuja,
ukivuma kutoka jangwani,
chemchemi yake haitatoa maji
na kisima chake kitakauka.
Ghala lake litatekwa
hazina zake zote.
16 qWatu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao,
kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao.
Wataanguka kwa upanga;
watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini,
wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”
Copyright information for SwhNEN