Hosea 8

Israeli Kuvuna Kisulisuli

1“Wekeni tarumbeta midomoni mwenu!
Tai yuko juu ya nyumba ya BWANA
kwa sababu watu wamevunja Agano langu,
wameasi dhidi ya sheria yangu.
2Israeli ananililia,
‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’
3Lakini Israeli amekataa lile lililo jema,
adui atamfuatia.
4Wanaweka Wafalme bila idhini yangu,
wamechagua wakuu bila kibali changu.
Kwa fedha zao na dhahabu
wamejitengenezea sanamu kwa ajili
ya maangamizi yao wenyewe.
5Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama!
Hasira yangu inawaka dhidi yao.
Watakuwa najisi mpaka lini?
6Zimetoka katika Israeli!
Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu.
Atavunjwa vipande vipande,
yule ndama wa Samaria.
7“Wanapanda upepo
na kuvuna upepo wa kisulisuli.
Bua halina suke,
halitatoa unga.
Kama lingetoa nafaka,
wageni wangeila yote.
8Israeli amemezwa;
sasa yupo miongoni mwa mataifa
kama kitu kisicho na thamani.
9Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru
kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake.
Efraimu amejiuza mwenyewe
kwa wapenzi.
10Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa,
sasa nitawakusanya pamoja.
Wataanza kudhoofika chini ya uonevu
wa mfalme mwenye nguvu.
11“Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi
kwa ajili ya sadaka za dhambi,
hizi zimekuwa madhabahu
za kufanyia dhambi.
12Nimeandika kwa ajili yao mambo mengi
kuhusu sheria yangu,
lakini wameziangalia
kama kitu cha kigeni.
13Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi
nao wanakula hiyo nyama,
lakini BWANA hapendezwi nao.
Sasa ataukumbuka uovu wao
na kuadhibu dhambi zao:
Watarudi Misri.
14Israeli amemsahau Muumba wake
na kujenga majumba ya kifalme,
Yuda amejengea miji mingi ngome.
Lakini nitatuma moto kwenye miji yao
utakaoteketeza ngome zao.”
Copyright information for Neno