Hosea 9

Adhabu Kwa Israeli

Usifurahie, Ee Israeli;
usishangilie kama mataifa mengine.
Kwa kuwa hukuwa
mwaminifu kwa Mungu wako;
umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu
ya kupuria nafaka.
Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai
havitalisha watu,
divai mpya itawapungukia.
Hawataishi katika nchi ya BWANA,
Efraimu atarudi Misri
na atakula chakula
kilicho najisi huko Ashuru.
Hawatammiminia BWANA sadaka ya divai
wala dhabihu zao hazitampendeza.
Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao
kama mkate wa waombolezaji;
nao wote wailao watakuwa najisi.
Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe;
kisije katika Hekalu la BWANA.
Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamuriwa,
katika siku za sikukuu za BWANA?
Hata ikiwa wataokoka maangamizi,
Misri atawakusanya,
nayo Memfisi
9.6 Memfisi kwa Kiebrania ni Nofu
itawazika.
Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma,
nayo miiba itafunika mahema yao.
Siku za adhabu zinakuja,
siku za malipo zimewadia.
Israeli na afahamu hili.
Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana
na uadui wenu ni mkubwa sana,
nabii anadhaniwa ni mpumbavu,
mtu aliyeongozwa na Mungu
anaonekana mwenda wazimu.
Nabii, pamoja na Mungu wangu,
ndiye mlinzi juu ya Efraimu,
hata hivyo mitego inamngojea
katika mapito yake yote,
na uadui katika nyumba ya Mungu wake.
Wamezama sana katika rushwa,
kama katika siku za Gibea.
Mungu atakumbuka uovu wao
na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.
10 “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama
kupata zabibu jangwani;
nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona
matunda ya kwanza katika mtini.
Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu
kwa ile sanamu ya aibu,
nao wakawa najisi
kama kitu kile walichokipenda.
11 Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege:
hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba,
hakuna kutunga mimba.
12 Hata wakilea watoto,
nitamwua kila mmoja.
Ole wao
nitakapowapiga kisogo!
13 Nimemwona Efraimu, kama Tiro,
aliyeoteshwa mahali pazuri.
Lakini Efraimu wataleta
watoto wao kwa mchinjaji.”
14 Wape, Ee BWANA,
je, utawapa nini?
Wape matumbo ya kuharibu mimba
na matiti yaliyokauka.
15 “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali,
niliwachukia huko.
Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi,
nitawafukuza katika nyumba yangu.
Sitawapenda tena,
viongozi wao wote ni waasi.
16 Efraimu ameharibiwa,
mzizi wao umenyauka,
hawazai tunda.
Hata kama watazaa watoto,
nitawachinja watoto wao
waliotunzwa vizuri.”
17 Mungu wangu atawakataa
kwa sababu hawakumtii;
watakuwa watu wa kutangatanga
miongoni mwa mataifa.
Copyright information for Neno