Isaiah 15

Unabii Dhidi Ya Moabu

Neno kuhusu Moabu: Ari iliyo katika Moabu imeangamizwa:
imeharibiwa kwa usiku mmoja!
Kiri iliyo katika Moabu imeangamizwa,
imeharibiwa kwa usiku mmoja!
Diboni anakwea hadi kwenye Hekalu lake,
mpaka mahali pake pa juu pa kuabudia miungu ili walie,
Moabu anaombolezea Nebo na Medeba.
Kila kichwa kimenyolewa
na kila ndevu zimeondolewa.
Wamevaa nguo za magunia barabarani,
juu ya mapaa na kwenye viwanja wote
wanaomboleza,
hulala kifudifudi kwa kulia.
Heshboni na Eleale wanalia,
sauti zao zinasikika hadi Yahasa.
Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu
wanapiga kelele,
nayo mioyo yao imezimia.
Moyo wangu unamlilia Moabu;
wakimbizi wake wanakimbilia Soari,
hadi Eglath-Shelishiya.
Wanapanda njia ya kwenda Luhithi,
wanakwenda huku wanalia;
kwenye barabara iendayo Horonaimu
wanaombolezea maangamizi yao.
Maji ya Nimrimu yamekauka
na majani yamenyauka;
mimea imekauka wala hakuna
kitu cho chote kibichi kilichobaki.
Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba
wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi.
Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu,
kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu,
maombolezo yao hadi Beer-Elimu.
Maji ya Dimoni yamejaa damu,
lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni:
simba juu ya wakimbizi wa Moabu
na juu ya wale wanaobaki katika nchi.


Copyright information for Neno