Isaiah 16

Hali Ya Kukata Tamaa Ya Moabu

Pelekeni wana-kondoo kama ushuru kwa mtawala wa nchi,
Kutoka Sela, kupitia jangwani, hadi mlima wa Binti Sayuni.
Kama ndege wanaopapatika waliofukuzwa kutoka kwenye kiota chao,
ndivyo walivyo wanawake wa Moabu
kwenye vivuko vya Arnoni.
“Tupeni shauri,
toeni uamuzi.
Wakati wa adhuhuri,
fanyeni kivuli chenu kama usiku.
Waficheni watoro,
msisaliti wakimbizi.
Waacheni watoro wa Moabu wakae pamoja nanyi;
iweni mahali pao pa salama
ili kuepuka mharabu.”
Mtesi atafikia mwisho
na maangamizi yatakoma,
aletaye vita atatoweka kutoka katika nchi.
Kwa upendo kiti cha enzi kitaimarishwa,
kwa uaminifu mtu ataketi juu yake,
yeye atokaye katika nyumba ya Daudi:
yeye ambaye katika kuhukumu hutafuta haki,
na huhimiza njia ya haki.
Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu,
kiburi chake cha kujivuna na udanganyifu,
kiburi chake na ufidhuli wake,
lakini majivuno yake si kitu.
Kwa hiyo Wamoabu wanaomboleza,
wanaiombolezea Moabu kwa pamoja.
Wanaomboleza na kuhuzunika
kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.
Mashamba ya Heshboni yananyauka,
pia na mizabibu ya Sibma.
Watawala wa mataifa
wamekanyaga mizabibu iliyo mizuri sana,
ambayo ilipata kufika Yazeri
na kuenea kuelekea jangwani.
Machipukizi yake yalienea
yakafika hadi baharini.
Hivyo ninalia kama Yazeri aliavyo,
kwa ajili ya mizabibu ya Sibma.
Ee Heshboni, Ee Eleale,
ninakulowesha kwa machozi!
Kelele za furaha kwa ajili ya tunda lako lililoiva
na kwa ajili ya mavuno zimekomeshwa.
10 Furaha na shangwe zimeondolewa
kutoka katika mashamba ya matunda;
hakuna ye yote aimbaye
wala apazaye sauti
katika mashamba ya mizabibu;
hakuna ye yote akanyagaye zabibu shinikizoni,
kwa kuwa nimekomesha makelele.
11 Moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama kinubi,
nafsi yangu yote kwa ajili ya Kir-Haresethi.
12 Wakati Moabu anapojitokeza mahali pake pa juu,
anajichosha mwenyewe tu;
anapokwenda mahali pake pa kuabudia miungu ili kuomba,
haitamfaidia lo lote.
13 

Hili ndilo neno ambalo BWANA ameshasema kuhusu Moabu.
14 Lakini sasa BWANA anasema: “Katika miaka mitatu, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, fahari ya Moabu na watu wake wengi watadharauliwa, nao walionusurika watakuwa wachache sana tena wanyonge.”

Copyright information for Neno