Isaiah 29

Ole Wa Mji Wa Daudi

Ole wako, wewe Arieli, Arieli,
mji alimokaa Daudi!
Ongezeni mwaka kwa mwaka
na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee.
Hata hivyo nitauzunguka Arieli kwa jeshi,
utalia na kuomboleza,
utakuwa kwangu kama mahali
pa kuwashia moto madhabahuni.
Nitapiga kambi pande zote dhidi yako,
nitakuzunguka kwa minara
na kupanga mazingiwa yangu dhidi yako.
Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini,
utamumunya maneno yako kutoka mavumbini.
Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu,
utanong'ona maneno yako toka mavumbini.
Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini,
kundi la wakatili watakuwa
kama makapi yapeperushwayo.
Naam, ghafula kwa mara moja,
BWANA Mwenye Nguvu Zote atakuja
na ngurumo, tetemeko la ardhi na kwa sauti kuu,
atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo.
Kisha makundi ya mataifa yote yale yapiganayo dhidi ya Arieli,
yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzunguka kwa jeshi,
watakuwa kama ilivyo ndoto,
kama maono wakati wa usiku:
kama vile wakati mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula,
lakini huamka, bado njaa yake ingalipo,
kama vile wakati mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji,
lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu.
Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa,
yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni.
Duwaa na kushangaa,
jifanyeni vipofu wenyewe na msione,
leweni, lakini si kwa mvinyo,
pepesukeni lakini si kwa kileo.
10 BWANA amewaleteeni juu yenu usingizi mzito:
Ameziba macho yenu (ninyi manabii);
amefunika vichwa vyenu (ninyi waonaji).
11 

Kwa maana kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa lakiri katika kitabu. Kama mkimpa mtu ye yote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa lakiri.”
12 Au kama mkimpa mtu ye yote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.”13 Bwana anasema: “Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao
na kuniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
Huniabudu bure,
mafundisho yao ni sheria tu
walizofundishwa na wanadamu.
14 Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa,
kwa ajabu juu ya ajabu,
hekima ya wenye hekima itapotea,
akili ya wenye akili itatoweka.”
15 Ole kwa wale wanaokwenda kwenye vilindi virefu
kumficha BWANA mipango yao,
wafanyao kazi zao gizani na kufikiri kuwa,
“Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?”
16 Mnapindua mambo juu chini,
kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi!
Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga,
“Wewe hukunifinyanga mimi?”
Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi,
“Wewe hujui cho chote?”
17 Kwa muda mfupi sana, je, Lebanoni haitageuzwa
kuwa shamba lenye rutuba
na shamba lenye rutuba liwe kama msitu?
18 Katika siku ile viziwi watasikia maneno ya kitabu
na katika utusitusi na giza macho ya kipofu yataona.
19 Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika BWANA,
wahitaji watafurahi katika yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
20 Wakatili watatoweka na wenye kudhihaki watatokomea,
nao wote wenye jicho la uovu watakatiliwa mbali,
21 wale ambao kwa neno humfanya mtu kuwa mwenye hatia,
wamtegeao mtego mtetezi katika mahakama
na kwa ushuhuda wa uongo humnyima haki
yeye asiye na hatia.22 Kwa hiyo hili ndilo BWANA, aliyemkomboa Abrahamu, analosema kwa nyumba ya Yakobo: “Yakobo hataaibishwa tena,
wala nyuso zao hazitabadilika sura tena.
23 Wakati watakapoona watoto wao miongoni mwao,
kazi ya mikono yangu,
watalitakasa Jina langu takatifu;
wataukubali utakatifu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Yakobo,
nao watamcha Mungu wa Israeli.
24 Wale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu,
wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.”


Copyright information for Neno