Isaiah 3

Hukumu Juu Ya Yerusalemu Na Yuda.

1Tazama sasa, Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote,
yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda
upatikanaji wa mahitaji na misaada,
upatikanaji wote wa chakula na maji,
2shujaa na mtu wa vita,
mwamuzi na nabii,
mwaguzi na mzee,
3jemadari wa kikosi cha watu hamsini
na mtu mwenye cheo, mshauri,
fundi stadi na mlozi mjanja.
4Nitawafanya wavulana wawe maafisa wao,
watoto ndio watakaowatawala.
5Watu wataoneana wao kwa wao
mtu dhidi ya mtu,
jirani dhidi ya jirani yake.
Kijana atainuka dhidi ya mzee,
mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.
6Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake
katika nyumba ya baba yake na kusema,
“Unalo joho, wewe uwe kiongozi wetu,
tawala lundo hili la magofu!”
7Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema,
“Sina uponyaji.
Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu,
msinifanye niwe kiongozi wa watu.”
8Yerusalemu inapepesuka,
Yuda inaanguka;
maneno yao na matendo yao ni kinyume na BWANA,
wakiudharau uwepo wake uliotukuka.
9Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao,
hujivunia dhambi yao kama Sodoma,
wala hawaifichi.
Ole wao!
Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.
10Waambie wanyofu itakuwa heri kwao,
kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.
11Ole wa watu waovu! Maafa yapo juu yao!
Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda.
12Vijana wanawatesa watu wangu,
wanawake wanawatawala.
Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,
wanawapoteza njia.
13BWANA anachukua nafasi yake mahakamani,
anasimama kuhukumu watu.
14BWANA anaingia katika hukumu
dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake:
“Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu,
mali zilizonyang'anywa kutoka kwa maskini
zimo nyumbani mwenu.
15Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu
na kuzisaga nyuso za maskini?”
asema Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote.

16BWANA asema,
“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,
wanatembea na shingo ndefu,
wakikonyeza kwa macho yao,
wakitembea kwa hatua fupi fupi za madaha,
wakiwa na mapambo yanayotoa mlio kwenye vifundo vya miguu yao.
17Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;
BWANA atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
18

Katika siku ile Bwana atawanyang'anya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo,
19vipuli, vikuku, shela, 20vilemba, mikufu ya kwenye vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi, 21pete zenye muhuri, pete za puani, 22majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha, 23vioo, mavazi ya kitani, taji na shali. 24Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo;
badala ya mishipi, kamba;
badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, upara;
badala ya mavazi mazuri, nguo za magunia;
badala ya uzuri, alama ya aibu kwa chuma cha moto.
25Wanaume wako watauawa kwa upanga,
mashujaa wako watauawa vitani.
26Malango ya Sayuni yataomboleza na kulia,
akiwa maskini, ataketi mavumbini.


Copyright information for Neno