Isaiah 37

Kuokolewa Kwa Yerusalemu Kunatabiriwa

1Wakati Mfalme Hezekia aliposikia hili, alirarua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda hekaluni mwa BWANA. 2Akawatuma Eliakimu msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu na makuhani viongozi, wote wakiwa wamevaa nguo ya gunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi. 3Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama vile wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa. 4Yamkini BWANA, Mungu wako atayasikia maneno ya Amirijeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo BWANA, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako hai.”

5Watumishi wa Mfalme Hezekia walipomjia Isaya, 6Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Usiogope kwa ajili ya yale uliyoyasikia, yale maneno ambayo kwayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana mimi. 7Sikiliza! Nitatia roho ndani yake ili kwamba atakaposikia taarifa fulani, atarudi katika nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’ ”

8Amirijeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi akamkuta mfalme anapigana dhidi ya Libna.

9Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anatoka kupigana dhidi yake. Aliposikia jambo hili akatuma wajumbe kwa Hezekia kwa neno hili: 10“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’ 11Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa? 12Je, miungu ya yale mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliwaokoa, miungu ya Gozani, Harani, Resefu na watu wa Edeni ambao walikuwa katika Telasari? 13Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”

Maombi Ya Hezekia

14Hezekia alipokea barua kutoka kwa wale wajumbe naye akaisoma. Kisha akapanda hekaluni mwa BWANA akaikunjua mbele za BWANA. 15Naye Hezekia akamwomba BWANA akisema: 16“Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Umeumba mbingu na nchi. 17Ee BWANA, tega sikio na usikie, fungua macho yako, Ee BWANA, uone, sikiliza maneno yote Senakeribu aliyotuma ili kumtukana Mungu aliye hai.

18“Ni kweli, Ee BWANA kwamba wafalme wa Waashuru wameyaangamiza mataifa haya yote pamoja na nchi zao. 19Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiteketeza, kwani haikuwa miungu bali ni miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 20Ee BWANA, Mungu wetu, sasa utuokoe toka mkononi mwake ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kwamba wewe peke yako, Ee BWANA, ndiwe Mungu.”

Kuanguka Kwa Senakeribu

21Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia akisema: “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: Kwa sababu umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru, 22hili ndilo neno ambalo BWANA amesema dhidi yake: “Bikira binti Sayuni
anakudharau na kukudhihaki.
Binti Yerusalemu
anatikisa kichwa chake ukimbiapo.
23Wewe ni nani uliyenitukana na kunikufuru?
Ni dhidi ya nani umeinua sauti yako
na kuinua macho yako kwa kiburi?
Ni dhidi ya yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!
24Kwa kutumia wajumbe wako
umelundika matukano juu ya Bwana.
Nawe umesema,
‘Kwa magari yangu mengi ya vita,
nimekwea kwenye vilele vya milima,
kwenye vilele vya juu kabisa vya Lebanoni.
Nimeikata mierezi yake iliyo mirefu kuliko yote,
misonobari yake iliyo bora sana.
Nimefika mahali pake palipoinuka palipo mbali sana,
katika msitu wake ulio mzuri kuliko yote.
25Nimechimba visima katika nchi za kigeni
na kuyanywa maji huko.
Kwa nyayo za miguu yangu
nimevikausha vijito vyote vya Misri.’
26“Je, hukusikia?
Zamani sana nililisimika.
Katika siku za zamani nililipanga,
na sasa nimelitimiza,
kwamba umeigeuza miji yenye maboma
kuwa malundo ya mawe.
27Watu wa miji hiyo, wakiwa wameishiwa nguvu,
wanatiwa hofu na kuaibishwa.
Wao ni kama mimea katika shamba,
kama machipukizi mororo ya kijani,
kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba,
ambayo hukauka kabla ya kukua.
28“Lakini ninajua mahali ukaapo,
kutoka kwako na kuingia kwako
na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
29Kwa sababu unaghadhibika na ufedhuli dhidi yangu
na kwa sababu ufidhuli wako umefika masikioni mwangu,
nitaweka ndoana yangu kwenye pua yako
na hatamu yangu kinywani mwako,
nami nitakufanya urudi kwa njia uliyoijia.30“Hii itakuwa ndiyo ishara kwako, Ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe
na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake.
Lakini katika mwaka wa tatu panda na kuvuna,
panda shamba la mizabibu
na ule matunda yake.
31Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda
yataeneza mizizi chini na kuzaa matunda.
32Kwa kuwa kutoka Yerusalemu yatatokea mabaki,
na kutoka Mlima Sayuni kikosi cha wale walionusurika.
Wivu wa BWANA Mwenye Nguvu Zote,
utatimiza hili.33“Kwa hiyo hili ndilo BWANA asemalo kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu
wala hatapiga mshale hapa.
Hatakuja mbele yake na ngao
wala kupanga majeshi kuzunguka dhidi yake.
34Kwa njia ile aliyoijia ndiyo atakayorudi kwayo;
hataingia katika mji huu,”
asema BWANA.

35“Nitaulinda mji huu na kuuokoa,
kwa ajili yangu mwenyewe
na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu!”36Ndipo malaika wa BWANA akaondoka na kuwaua watu mia themanini na tano elfu katika kambi ya Waashuru. Watu walipoamka asubuhi yake, wote huko walikuwa maiti! 37Kwa hiyo Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Alirudi Ninawi na kukaa huko.

38Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza walimwua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.

Copyright information for Neno