Isaiah 38

Kuugua Kwa Mfalme Hezekia

Katika siku hizo Hezekia akaugua naye akawa karibu na kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akamwendea na kumwambia, “Hili ndilo asemalo BWANA: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”

Hezekia akageuza uso wake kuelekea ukutani na kumwomba BWANA, “Ee BWANA, kumbuka, jinsi nilivyotembea mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wote nami nimefanya lile lililo jema machoni pako.” Naye Hezekia akalia sana sana.

Ndipo neno la BWANA likamjia Isaya: “Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa baba yako Daudi: Nimesikia maombi yako na nimeona machozi yako, nitaiongeza miaka kumi na mitano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka katika mkono wa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu.

“ ‘Hii ndiyo ishara ya BWANA kwako ya kwamba BWANA atafanya kile alichoahidi: Nitafanya kivuli cha jua kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi kirudi nyuma madaraja kumi.’ ” Hivyo jua likarudi nyuma madaraja kumi ambayo lilikuwa limeshuka.



Maandiko ya Hezekia mfalme wa Yuda baada ya kuugua kwake na kupona: 10 Nilisema, “Katika ustawi wa maisha yangu
je, ni lazima nipite katika malango ya mauti
38.10 Mauti hapa maana yake ni Kuzimu

na kupokonywa miaka yangu iliyobaki?”
11 Nilisema, “Sitamwona tena BWANA,
BWANA katika nchi ya walio hai,
wala sitamtazama tena mwanadamu,
wala kuwa na wale ambao sasa wanakaa katika ulimwengu huu.
12 Kama hema la mchunga mifugo,
nyumba yangu imebomolewa na kutwaliwa kutoka kwangu.
Kama mfumaji nimevingirisha maisha yangu,
naye amenikatilia mbali kutoka kitanda cha mfumi,
mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
13 Nilingoja kwa uvumilivu hadi mapambazuko,
lakini kama simba alivunja mifupa yangu yote,
mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
14 Nililia kama mbayuwayu au korongo,
niliomboleza kama hua aombolezaye.
Macho yangu yalififia nilipotazama mbinguni.
Ee Bwana, ninataabika, njoo unisaidie!”
15 Lakini niseme nini?
Amesema nami,
naye yeye mwenyewe amelitenda hili.
Nitatembea kwa unyenyekevu
katika miaka yangu yote
kwa sababu ya haya maumivu makali
ya nafsi yangu.
16 Bwana, kwa mambo kama haya watu huishi,
nayo roho yangu hupata uzima katika hayo pia.
Uliniponya
na kuniacha niishi.
17 Hakika ilikuwa kwa ajili ya faida yangu ndiyo maana nikapata maumivu makali.
Katika upendo wako ukaniokoa
kutoka katika shimo la uharibifu;
umeziweka dhambi zangu zote
nyuma yako.
18 Kwa maana kaburi
38.18 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol
haliwezi kukusifu,
mauti haiwezi kuimba sifa zako;
wale washukao chini shimoni
hawawezi kuutarajia uaminifu wako.
19 Walio hai, walio hai, wanakusifu,
kama ninavyofanya leo;
baba huwaambia watoto wao
habari za uaminifu wako.
20 BWANA ataniokoa,
nasi tutaimba kwa vyombo vya nyuzi
siku zote za maisha yetu
katika Hekalu la BWANA.



21 Isaya alikuwa amesema, “Uandae mkate wa tini uubandike juu ya jipu, naye atapona.”

22 Hezekia alikuwa ameuliza, “Ni ishara ipi kwamba nitapanda kwenda hekaluni mwa BWANA?”

Copyright information for Neno