Isaiah 42

Mtumishi Wa BWANA

1“Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,
mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye;
nitaweka Roho yangu juu yake,
naye ataleta haki kwa mataifa.
2Hatapaza sauti wala kupiga kelele,
wala hataiinua sauti yake barabarani.
3mwanzi uliopondeka hatauvunja
na utambi ufukao moshi hatauzima.
Kwa uaminifu ataleta haki,
4hatazimia roho wala kukata tamaa
mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia.
Visiwa vitaweka tumaini lake katika sheria yake.”
5Hili ndilo asemalo Mungu, BWANA,
yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,
aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo,
awapaye watu wake pumzi
na uzima kwa wale waendao humo:
6“Mimi, BWANA, nimekuita katika haki;
nitakushika mkono wako.
Nitakulinda na kukufanya
kuwa Agano kwa ajili ya watu
na nuru kwa Mataifa,
7kuwafungua macho wale wasioona,
kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela,
na kuwafungua kutoka gerezani
wale wanaokaa gizani.
8“Mimi ndimi BWANA; hilo ndilo Jina langu!
Sitampa mwingine utukufu wangu
wala sanamu sifa zangu.
9Tazama, mambo ya kwanza yametokea,
nami natangaza mambo mapya;
kabla hayajatokea
nawatangazia habari zake.”

Wimbo Wa Kumsifu BWANA

10Mwimbieni BWANA wimbo mpya,
sifa zake toka miisho ya dunia,
ninyi mshukao chini baharini,
na vyote vilivyomo ndani yake,
enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.
11Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;
makao anamoishi Kedari na yashangilie.
Watu wa Sela waimbe kwa furaha
na wapige kelele kutoka vilele vya milima.
12Wampe BWANA utukufu
na kutangaza sifa zake katika visiwa.
13BWANA ataenda kama mtu mwenye nguvu,
kama shujaa atachochea shauku yake,
kwa kelele ataamsha kilio cha vita
naye atashinda adui zake.
14“Kwa muda mrefu nimenyamaza kimya,
nimekaa kimya na kujizuia.
Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua,
ninapiga kelele, ninatweta
na kushusha pumzi.
15Nitaharibu milima na vilima
na kukausha uoto wake wote;
nitafanya mito kuwa visiwa
na kukausha mabwawa.
16Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua,
kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza;
nitafanya giza kuwa nuru mbele yao
na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini.
Haya ndiyo mambo nitakayofanya;
mimi sitawaacha.
17Lakini wale wanaotumaini sanamu,
wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’
watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.

Israeli Kipofu Na Kiziwi

18“Sikieni, enyi viziwi;
tazameni, enyi vipofu, mpate kuona!
19Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu,
na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma?
Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu,
aliye kipofu kama mtumishi wa BWANA?
20Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia;
masikio yenu yako wazi lakini hamsikii cho chote.”
21Ilimpendeza BWANA
kwa ajili ya haki yake
kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu.
22Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara,
wote wamenaswa katika mashimo,
au wamefichwa katika magereza.
Wamekuwa nyara,
wala hapana ye yote awaokoaye.
wamefanywa mateka,
wala hapana ye yote asemaye, “Warudishe.”
23Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili
au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao?
24Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka,
na Israeli kwa wateka nyara?
Je, hakuwa BWANA,
ambaye tumetenda dhambi dhidi yake?
Kwa kuwa hawakufuata njia zake,
hawakutii sheria zake.
25Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka,
ukali wa vita.
Ikawazunguka kwa miali ya moto,
hata hivyo hawakuelewa;
ikawateketeza,
lakini hawakuyatia moyoni.
Copyright information for Neno