Isaiah 43

Mwokozi Pekee Wa Israeli

1Lakini sasa hili ndilo asemalo BWANA,
yeye aliyekuumba, Ee Yakobo,
yeye aliyekuhuluku, Ee Israeli:
“Usiogope kwa maana nimekukomboa,
nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.
2Unapopita kwenye maji makuu,
nitakuwa pamoja nawe,
unapopita katika mito ya maji,
hayatakugharikisha.
Utakapopita katika moto,
hutaungua,
miali ya moto haitakuunguza.
3Kwa kuwa Mimi ndimi BWANA, Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako,
ninaitoa Misri kuwa fidia yako,
Kushi na Seba badala yako.
4Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,
nami kwa kuwa ninakupenda,
nitatoa watu badala yako
na mataifa badala ya maisha yako.
5Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe,
nitawaleta watoto wako kutoka mashariki
na kukukusanya kutoka magharibi.
6Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’
nayo kusini, ‘Usiwazuie.’
Walete wana wangu kutoka mbali
na binti zangu kutoka miisho ya dunia:
7kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu,
niliyemwumba kwa utukufu wangu,
niliyemhuluku na kumfanya.”
8Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni,
wenye masikio lakini hawasikii.
9Mataifa yote yanakutanika pamoja
na mataifa wanakusanyika.
Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya
na kututangazia mambo yaliyopita?
Walete mashahidi wao ili kuthibitisha kuwa walikuwa sahihi,
ili kwamba wengine waweza kusikia na kusema, “Ni kweli.”
10“Ninyi ni mashahidi wangu,” asema BWANA,
“na mtumishi wangu niliyemchagua,
ili mpate kunijua na kuniamini
na kutambua kwamba Mimi ndiye.
Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa,
wala hatakuwepo mwingine baada yangu.
11Mimi, naam mimi, ndimi BWANA,
zaidi yangu hakuna mwokozi.
12Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza:
Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu.
Ninyi ni mashahidi wangu,” asema BWANA,
“kwamba Mimi ndimi Mungu.
13Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye.
Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa
kutoka katika mkono wangu.
Mimi ninapotenda,
ni nani awezaye kutangua?”

Huruma Za Mungu Na Kukosa Uaminifu Kwa Israeli

14Hili ndilo BWANA asemalo,
Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:
“Kwa ajili yenu nitatumana Babeli
na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi,
katika meli walizozionea fahari.
15Mimi ndimi BWANA, yeye Aliye Mtakatifu wako,
Muumba wa Israeli, Mfalme wako.”
16Hili ndilo asemalo BWANA,
yeye aliyefanya njia baharini,
mahali pa kupita kwenye maji mengi,
17aliyeyakokota magari ya vita na farasi,
jeshi pamoja na askari wa msaada,
nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe,
wamekomeshwa, wakazimika kama utambi:
18“Msiyakumbuke mambo yaliyopita,
wala msiyatafakari mambo ya zamani.
19Tazama, nitafanya jambo jipya!
Sasa litachipuka, je, hamtalitambua?
Nitafanya njia jangwani
na vijito vya maji katika nchi kame.
20Wanyama wa mwituni wataniheshimu,
mbweha na bundi,
kwa sababu ninawapatia maji jangwani,
na vijito katika nchi kame,
ili kuwapa watu wale maji, ambao ni chaguo langu.
21Watu wale niliowaumba kwa ajili yangu,
ili wapate kutangaza sifa zangu.
22“Hata hivyo hukuniita mimi, Ee Yakobo,
hujajitaabisha kwa ajili yangu, Ee Israeli.
23Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa,
wala kuniheshimu kwa dhabihu zako.
Sikukulemea kwa sadaka za nafaka
wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba.
24Hukuninunulia uvumba wo wote wenye manukato,
wala hukunipa kwa ukarimu
mafuta ya wanyama wa dhabihu zako.
Lakini umenilemea kwa dhambi zako
na kunitaabisha kwa makosa yako.
25“Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako,
kwa ajili yangu mwenyewe,
wala sizikumbuki dhambi zako tena.
26Tafakari mambo yaliyopita,
njoo na tuhojiane,
leta shauri lako, uweze kupewa haki yako.
27Baba yako wa kwanza, alitenda dhambi,
wasemaji wako wameasi dhidi yangu.
28Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako,
nami nitamtoa Yakobo aangamizwe
na Israeli adhihakiwe.
Copyright information for Neno