Isaiah 44

Israeli Aliyechaguliwa

1“Lakini sasa sikiliza, Ee Yakobo, mtumishi wangu,
Israeli, niliyemchagua.
2Hili ndilo asemalo BWANA,
yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni,
yeye atakayekusaidia:
Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu,
Yeshuruni
44.2 Yeshuruni hapa maana yake ni Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli (ona pia Kum 32:15)
, niliyekuchagua.
3Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu
na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka;
nitamimina Roho wangu juu ya watoto wako,
nayo baraka yangu juu ya wazao wako.
4Nao watachipua kama manyasi katika shamba la majani,
kama mierezi kando ya vijito vya maji yatiririkayo.
5Mmoja atasema, ‘Mimi ni wa BWANA’;
mwingine atajiita kwa jina la Yakobo;
vile vile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘Wa BWANA,’
na kujiita kwa jina la Israeli.

Ni BWANA, Siyo Sanamu

6“Hili ndilo asemalo BWANA,
Mfalme wa Israeli na Mkombozi,
BWANA Mwenye Nguvu Zote:
Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho;
zaidi yangu hakuna Mungu.
7Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na aseme.
Yeye na aseme na kuweka mbele yangu
ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale,
tena ni nini kitakachotokea,
naam, yeye na atoa unabii ni nini kitakachokuja.
8Msitetemeke, msiogope.
Je, sikutangaza hili na kutoa unabii tangu zamani?
Ninyi ni mashahidi wangu.
Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi?
Hasha, hakuna Mwamba mwingine;
mimi simjui mwingine.”
9Wote wachongao sanamu ni ubatili,
navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.
Wale ambao wangesema juu yao ni vipofu,
ni wajinga, ili wao waaibike.
10Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,
ambayo haiwezi kumfaidia kitu cho chote?
11Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,
mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.
Wote na wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,
watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.
12Muhunzi huchukua kifaa
na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto,
hutengeneza sanamu kwa nyundo,
huifanyiza kwa nguvu za mkono wake.
Huona njaa na kupoteza nguvu zake,
asipokunywa maji huzimia.
13Seremala hupima kwa kutumia kamba
na huuchora mstari kwa kalamu;
huchonga kwa patasi
na kutia alama kwa bikari.
Huifanyiza katika umbo la binadamu,
la mwanadamu katika utukufu wake wote,
ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu.
14Hukata miti ya mierezi,
huchukua mteashuri au mwaloni.
Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni,
au hupanda msunobari, mvua huufanya ukue.
15Ni kuni kwa ajili ya binadamu,
huchukua baadhi yake na kuota moto,
huwasha moto na kuoka mkate.
Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu,
huitengeneza sanamu na kuisujudia.
16Sehemu ya kuni huziweka motoni,
akapikia chakula chake,
hubanika nyama na kula hadi ashibe.
Huota moto na kusema,
“Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”
17Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake;
yeye huisujudia na kuiabudu.
Huiomba na kusema,
“Niokoe; wewe ni mungu wangu.”
18Hawajui cho chote, hawaelewi cho chote,
macho yao yamefungwa hivyo hawawezi kuona,
akili zao zimefungwa hivyo hawawezi kufahamu.
19Wala hakuna anayefikiri,
hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema,
“Sehemu yake nilitumia kwa kuni;
hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake,
nilibanika nyama na kuila.
Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki?
Je, nisujudie gogo la mti?”
20Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha;
hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema,
“Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?”
21“Ee Yakobo, kumbuka mambo haya,
Ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu.
Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu,
Ee Israeli, sitakusahau.
22Nimeyafuta makosa yako kama wingu,
dhambi zako kama ukungu wa asubuhi.
Nirudie mimi,
kwa kuwa nimekukomboa wewe.”
23Enyi mbingu, imbeni kwa furaha,
kwa maana BWANA amefanya jambo hili,
Ee vilindi vya dunia, piga kelele.
Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo,
enyi misitu na miti yenu yote,
kwa maana BWANA amemkomboa Yakobo,
ameuonyesha utukufu wake katika Israeli.

Yerusalemu Kukaliwa

24“Hili ndilo asemalo BWANA,
Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni:
“Mimi ni BWANA,
yeye aliyeumba vitu vyote,
yeye peke yake aliyezitanda mbingu,
yeye aliyeitandaza nchi mwenyewe,
25“yeye huzipinga ishara za manabii wa uongo,
na kuwatia upumbavu waaguzi,
ayapinduaye maarifa ya wenye hekima,
na kuyafanya kuwa upuzi,
26ayathibitishaye maneno ya watumishi wake,
na kutimiza utabiri wa wajumbe wake,
“yeye aiambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’
aiambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’
na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’
27akiambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka,
nami nitakausha vijito vyako,’
28amwambiaye Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu,
naye atatimiza yote yanipendezayo;
atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,”
na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’
Copyright information for Neno