Isaiah 45

Koreshi Chombo Cha Mungu

“Hili ndilo asemalo BWANA kwa mpakwa mafuta wake,
Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume
kutiisha mataifa mbele yake
na kuwavua wafalme silaha zao,
kufungua milango mbele yake
ili kwamba malango yasije yakafungwa:
Nitakwenda mbele yako
na kusawazisha milima;
nitavunjavunja malango ya shaba
na kukatakata mapingo ya chuma.
Nitakupa hazina za gizani,
mali zilizofichwa mahali pa siri,
ili upate kujua ya kwamba Mimi ndimi BWANA,
Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako.
Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu,
Israeli niliyemchagua,
nimekuita wewe kwa jina lako
na kukupa jina la heshima,
ingawa wewe hunitambui.
Mimi ndimi BWANA, wala hakuna mwingine,
zaidi yangu hakuna Mungu.
Nitakutia nguvu,
ingawa wewe hukunitambua,
ili kwamba kutoka maawio ya jua
mpaka machweo yake,
watu wapate kujua kwamba
hakuna Mungu mwingine ila Mimi.
Mimi ndimi BWANA wala hakuna mwingine.
Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza,
ninaleta mafanikio na kusababisha maafa,
Mimi, BWANA, hufanya vitu hivi vyote.
“Enyi mbingu juu, nyesheni haki,
mawingu na yaidondoshe.
Dunia na ifunguke sana,
wokovu na uchipuke,
haki na ikue pamoja nao;
mimi, BWANA, ndiye niliyeiumba.
“Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake,
yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi.
Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi,
‘Unatengeneza nini wewe?’
Je, kazi yako husema,
‘Hana mikono’?
10 Ole wake amwambiaye baba yake,
‘Umezaa nini?’
Au kumwambia mama yake,
‘Umezaa kitu gani?’
11 “Hili ndilo asemalo BWANA,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake:
Kuhusu mambo yatakayokuja,
je, unaniuliza habari za watoto wangu,
au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?
12 Mimi ndiye niliyeumba dunia
na kumwumba mwanadamu juu yake.
Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu,
nikayapanga majeshi yake yote ya angani.
13 Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu:
Nitazinyosha njia zake zote.
Yeye atajenga kwa upya mji wangu
na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni,
lakini si kwa kima cha fedha wala kwa kupewa zawadi,
asema BWANA Mwenye Nguvu Zote.”
14 

Hili ndilo asemalo BWANA: “Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi,
nao wale Waseba warefu,
watakujia na kuwa wako,
watakujia wakijikokota nyuma yako,
watakujia wamefungwa minyororo.
Watasujudu mbele yako
wakikusihi na kusema,
‘Hakika Mungu yu pamoja nawe,
wala hakuna mwingine;
hakuna Mungu mwingine.’ ”
15 Hakika wewe u Mungu unayejificha,
Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli.
16 Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika;
watatahayarika kwa pamoja.
17 Lakini Israeli ataokolewa na BWANA
kwa wokovu wa milele;
kamwe hutaaibika wala kutatahayarika,
milele yote.
18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA,
yeye aliyeumba mbingu,
ndiye Mungu;
yeye aliyeifanya dunia na kuiumba,
yeye ndiye aliyeiwekea misingi imara,
hakuiumba ili iwe tupu,
bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake,
anasema:
“Mimi ndimi BWANA,
wala hakuna mwingine.
19 Sijasema sirini,
kutoka mahali fulani katika nchi ya giza;
sijawaambia wazao wa Yakobo,
‘Nitafuteni bure.’
Mimi, BWANA, nasema kweli;
ninatangaza lile lililo sahihi.
20 “Kusanyikeni pamoja mje,
enyi wakimbizi kutoka katika mataifa.
Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili,
Wale waombao miungu ile isiyoweza kuokoa.
21 Tangazeni lile litakalokuwapo, lisemeni hilo,
wao na wafanye shauri pamoja.
Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani,
aliyetangaza tangu zamani za kale?
Je, haikuwa Mimi, BWANA?
Wala hapana Mungu mwingine
zaidi yangu mimi,
Mungu mwenye haki na Mwokozi;
hapana mwingine ila mimi.
22 “Nigeukieni mimi nanyi mkaokolewe,
enyi miisho yote ya dunia;
kwa maana mimi ndimi Mungu,
wala hapana mwingine.
23 Nimeapa kwa nafsi yangu,
kinywa changu kimenena katika uadilifu wote
neno ambalo halitatanguka:
Kila goti litapigwa mbele zangu,
kwangu mimi kila ulimi utaapa.
24 Watasema kuhusu mimi,
‘Katika BWANA peke yake
ndiko kuna haki na nguvu.’ ”
Wote ambao wamemkasirikia Mungu
watamjia yeye nao watatahayarika.
25 Lakini katika BWANA wazao wote wa Israeli
wataonekana wenye haki na kutukuka.


Copyright information for Neno