Isaiah 46

Miungu Ya Babeli

1Beli anasujudu hadi nchi, Nebo anainama;
sanamu zao hubebwa na wanyama wa mizigo.
Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea,
mzigo kwa waliochoka.
2Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini;
hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu,
wote wanakwenda utumwani pamoja.
3“Nisikilizeni mimi, Ee nyumba ya Yakobo,
ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli,
ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba,
nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.
4Hata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi Mimi ndiye,
Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.
Nimewahuluku nami nitawabeba,
nitawasaidia ninyi na kuwaokoa.
5“Mtanilinganisha na nani
au mtanihesabu kuwa sawa na nani?
Ni nani mtakayenifananisha naye
ili tuweze kulinganishwa?
6Wengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao
na kupima fedha kwenye mizani;
huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,
kisha huisujudia na kuiabudu.
7Huiinua kuiweka mabegani na kuichukua;
huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo,
wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.
Ingawa mtu huililia, haijibu;
haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.
8“Kumbukeni hili, mkajionyesha kuwa waume,
litieni akilini, liwekeni moyoni, enyi waasi.
9Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;
mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;
mimi ndimi Mungu,
wala hakuna mwingine aliye kama mimi.
10Ni mimi tangazaye mwisho tangu mwanzo,
naam, tangu zamani za kale,
mambo ambayo hayajatendeka.
Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,
nami nitatenda mapenzi yangu yote.
11Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;
kutoka nchi ya mbali,
mtu atakayetimiza kusudi langu.
Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;
lile nililolipanga, hilo ndilo nitakalolitenda.
12Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,
ninyi mlio mbali na haki.
13Ninaleta haki yangu karibu,
haiko mbali;
wala wokovu wangu hautachelewa.
Nitawapa Sayuni wokovu,
Israeli utukufu wangu.
Copyright information for Neno