Isaiah 5

Wimbo Wa Shamba La Mizabibu

1Nitaimba wimbo kwa ajili ya mmoja nimpendaye
kuhusu shamba lake la mizabibu:
Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu
kwenye kilima chenye rutuba.
2Alililima na kuondoa mawe
na akaliotesha mizabibu bora sana.
Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake
na kutengeneza shinikizo la kukamulia divai pia.
Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri,
lakini lilizaa matunda mabaya tu.
3“Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda,
hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu.
4Ni nini zaidi ambacho kingeweza kufanyika
kwa ajili ya shamba langu la mizabibu
kuliko yale niliyofanya?
Nilipotazamia kupata zabibu nzuri,
kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu?
5Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea
shamba langu la mizabibu:
Nitaondoa uzio wake,
nalo litaharibiwa,
nitabomoa ukuta wake,
nalo litakanyagwa.
6Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu,
halitakatiwa matawi wala kulimwa,
nayo michongoma na miiba itamea huko,
nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”
7Shamba la mzabibu la BWANA Mwenye Nguvu Zote
ni nyumba ya Israeli,
na watu wa Yuda
ni bustani yake ya kumpendeza.
Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu,
alitazamia uadilifu,
lakini akasikia vilio vya taabu.

Ole Na Hukumu

8Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba
na kuunganisha mashamba baada ya mashamba
hadi hakuna nafasi iliyobaki
nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.
9BWANA Mwenye Nguvu Zote amesema nikisikia:
“Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa,
nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.
10Shamba la mizabibu la eka kumi
litatoa bathi
5.10 Bathi moja ni sawa na lita 22
moja ya divai,
na homeri
5.10 Homeri moja ni sawa na lita 220
ya mbegu zilizopandwa
itatoa efa
5.10 Efa moja ni sawa na lita 22
moja tu ya nafaka.”
11Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema
wakikimbilia kunywa vileo,
wale wakawiao sana mpaka usiku,
mpaka wamewaka kwa mvinyo.
12Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao,
matari, filimbi na mvinyo,
lakini hawayajali matendo ya BWANA,
wala hawana heshima
kwa ajili ya kazi ya mikono yake.
13Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni
kwa sababu ya kukosa ufahamu,
watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa
na watu wao wengi watakauka kwa kiu.
14Kwa hiyo kaburi
5.14 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol
limeongeza hamu yake
na kupanua mdomo wake bila kikomo,
ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu
pamoja na wagomvi wao
na wafanyao sherehe wote.
15Hivyo mwanadamu atashushwa
na binadamu atanyenyekezwa,
macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.
16Lakini BWANA Mwenye Nguvu Zote atatukuzwa
kwa ajili ya haki yake,
naye Mungu Mtakatifu atajionyesha mwenyewe
kuwa mtakatifu kwa haki yake.
17Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe,
wana-kondoo na wageni watajilisha
katika magofu ya matajiri.
18Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu
na uovu kama kwa kamba za mkokoteni,
19kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka,
aharakishe kazi yake
ili tupate kuiona.
Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike,
tena udhihirike ili tupate kuujua.”
20Ole wao wanaoita ubaya ni wema
na wema ni ubaya,
wawekao giza badala ya nuru
na nuru badala ya giza,
wawekao uchungu badala ya utamu
na utamu badala ya uchungu.
21Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe
na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.
22Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo
nao walio hodari katika kuchanganya vileo,
23wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo,
lakini huwanyima haki wasio na hatia.
24Kwa hiyo, kama ndimi za moto zirambavyo nyasi
na kama vile majani makavu
yazamavyo katika miali ya moto,
ndivyo mizizi yao itakavyooza
na maua yao yatakavyopeperushwa
kama mavumbi;
kwa kuwa wameikataa sheria ya BWANA Mwenye Nguvu Zote
na kulisukumia mbali
neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli.
25Kwa hiyo hasira ya BWANA inawaka dhidi ya watu wake,
mkono wake umeinuliwa na anawapiga.
Milima inatetemeka,
maiti ni kama takataka kwenye barabara.
Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.
26Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali,
anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia.
Tazama wamekuja,
kwa kasi na kwa haraka!
27Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa,
hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala,
hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni,
hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika.
28Mishale yao ni mikali,
pinde zao zote zimevutwa,
kwato za farasi wao ziko kama jiwe la gumegume,
magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli.
29Ngurumo yao ni kama ile ya simba,
wananguruma kama wana simba,
wanakoroma wanapokamata mawindo yao
na kuondoka nayo pasipo ye yote wa kuokoa.
30Katika siku ile watanguruma juu yake
kama ngurumo za bahari.
Kama mtu akiitazama nchi,
ataona giza na dhiki;
hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.
Copyright information for Neno