Jeremiah 21

Mungu Anakataa Ombi La Sedekia

1 aNeno lilimjia Yeremia kutoka kwa Bwana wakati Mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkiya, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwake, kusema: 2 b“Tuulizie sasa kwa Bwana, kwa sababu Nebukadneza mfalme wa Babeli anatushambulia. Labda Bwana atatenda maajabu kwa ajili yetu kama nyakati zilizopita, ili Nebukadneza atuondokee.”

3Lakini Yeremia akawajibu, “Mwambieni Sedekia, 4 c‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kuwageuzia silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo mnatumia kupigana na mfalme wa Babeli na Wakaldayo ambao wako nje ya ukuta wakiwazunguka kwa jeshi. Nami nitawakusanya ndani ya mji huu. 5 dMimi mwenyewe nitapigana dhidi yenu kwa mkono wangu ulionyooshwa na mkono wa nguvu, kwa hasira na ghadhabu kali na ukali mwingi. 6 eNitawaangamiza waishio katika mji huu, watu na wanyama, nao watauawa kwa tauni ya kutisha. 7 fBaada ya hayo, nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake na watu wa mji huu ambao walinusurika tauni, upanga na njaa, mkononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, na kwa adui zao wale wanaotafuta uhai wao. Atawaua kwa upanga; hatakuwa na rehema juu yao au huruma wala kuwasikitikia,’ asema Bwana.

8“Zaidi ya hayo, waambie watu hawa, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Tazama, naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti. 9 gYeyote atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni. Lakini yeyote atakayetoka na kujisalimisha kwa Wakaldayo ambao wameuzunguka mji huu kwa jeshi, atanusurika, naye ataishi. 10 hNimekusudia kuufanyia mji huu jambo baya, wala si jema. Utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto, asema Bwana.’

11 i“Zaidi ya hayo, ambia nyumba ya mfalme ya Yuda, ‘Sikia neno la Bwana, 12 jEwe nyumba ya Daudi, hili ndilo Bwana asemalo:

“ ‘Hukumuni kwa haki kila asubuhi,
mwokoeni mikononi mwa mdhalimu
yeye aliyetekwa nyara,
la sivyo ghadhabu yangu italipuka
na kuwaka kama moto
kwa sababu ya uovu mlioufanya:
itawaka na hakuna wa kuizima.
13 kNiko kinyume nawe, ee Yerusalemu,
wewe uishiye juu ya bonde hili
kwenye uwanda wa juu wa miamba,
asema Bwana,
wewe usemaye, “Ni nani awezaye kuja kinyume chetu?
Nani ataingia mahali pa kimbilio letu?”
14 lNitawaadhibu kama istahilivyo matendo yenu,
asema Bwana.
Nitawasha moto katika misitu yenu
ambao utateketeza kila kitu kinachowazunguka.’ ”
Copyright information for SwhNEN