Jeremiah 23

Tawi La Haki

1 a“Ole wao wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu!” asema Bwana. 2 bKwa hiyo hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, analowaambia wachungaji wanaowachunga watu wangu: “Kwa sababu mmelitawanya kundi langu na kuwafukuzia mbali, wala hamkuwatunza, basi mimi nitawaadhibu kwa ajili ya uovu mliofanya,” asema Bwana. 3 c“Mimi mwenyewe nitayakusanya mabaki ya kundi langu kutoka nchi zote ambazo nimewafukuzia, nami nitawarudisha katika malisho yao, mahali ambapo watazaa na kuongezeka idadi yao. 4 dNitaweka wachungaji juu yao ambao watawachunga, nao hawataogopa tena au kutishwa, wala hatapotea hata mmoja,” asema Bwana.

5 e Bwana asema, “Siku zinakuja,
nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,
Mfalme atakayetawala kwa hekima,
na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.
6 fKatika siku zake, Yuda ataokolewa
na Israeli ataishi salama.
Hili ndilo jina atakaloitwa:
Bwana Haki Yetu.
7 g“Hivyo basi, siku zinakuja, wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’ 8 hbali watasema, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewatoa wazao wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia,’ asema Bwana. Ndipo wataishi katika nchi yao wenyewe.”

Manabii Wasemao Uongo

9 iKuhusu manabii:

Moyo wangu umevunjika ndani yangu;
mifupa yangu yote inatetemeka.
Nimekuwa kama mtu aliyelewa,
kama mtu aliyelemewa na divai,
kwa sababu ya Bwana
na maneno yake matakatifu.
10 jNchi imejaa wazinzi;
kwa sababu ya laana, nchi imekauka
na malisho yaliyoko nyikani yamekauka.
Mwenendo wa manabii ni mbaya
na mamlaka yao si ya haki.

11 k“Nabii na kuhani wote si wacha Mungu;
hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,”
asema Bwana.
12 l“Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi,
watafukuziwa mbali gizani
na huko wataanguka.
Nitaleta maafa juu yao
katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,”
asema Bwana.

13 m“Miongoni mwa manabii wa Samaria
nililiona jambo la kuchukiza:
Walitabiri kwa Baali
na kuwapotosha Israeli watu wangu.
14 nNako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu
nimeona jambo baya sana:
Wanafanya uzinzi
na kuenenda katika uongo.
Wanatia nguvu mikono ya watenda mabaya,
kwa ajili hiyo hakuna yeyote
anayeachana na uovu wake.
Wote wako kama Sodoma kwangu;
watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”
15 oKwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo kuhusu manabii:

“Nitawafanya wale chakula kichungu
na kunywa maji yaliyotiwa sumu,
kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu
kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”
16 pHili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:

“Msisikilize wanachowatabiria manabii,
wanawajaza matumaini ya uongo.
Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe,
hayatoki katika kinywa cha Bwana.
17 qHuendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi,
Bwana asema: Mtakuwa na amani.’
Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao,
wao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’
18 rLakini ni yupi miongoni mwao aliyesimama katika baraza la Bwana
ili kuona au kusikia neno lake?
Ni nani aliyesikiliza
na kusikia neno lake?
19 sTazama, dhoruba ya Bwana
itapasuka kwa ghadhabu,
kisulisuli kitazunguka na kuanguka
vichwani vya waovu.
20 tHasira ya Bwana haitageuka mpaka amelitimiza kusudi la moyo wake.
Siku zijazo mtalifahamu kwa wazi.
21 uMimi sikuwatuma manabii hawa,
lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao.
Mimi sikusema nao,
lakini wametabiri.
22 vLakini kama wangesimama barazani mwangu,
wangetangaza maneno yangu kwa watu wangu,
nao wangewageuza kutoka njia zao mbaya
na kutoka matendo yao maovu.”

23 w“Je, mimi ni Mungu aliyeko hapa karibu tu,”
Bwana asema,
“wala si Mungu aliyeko pia mbali?
24 xJe, mtu yeyote aweza kujificha
mahali pa siri ili nisiweze kumwona?”
Bwana asema.
“Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?”
Bwana asema.
25 y“Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’ 26 zMambo haya yataendelea mpaka lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe? 27 aaWanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau jina langu kwa kumwabudu Baali. 28 abMwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Bwana. 29 ac“Je, neno langu si kama moto,” asema Bwana, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?

30 ad“Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asema Bwana. 31“Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotikisa ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Bwana asema.’ 32 aeKweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Bwana. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Bwana.

Maneno Ya Uongo Na Manabii Wa Uongo

33 af“Wakati watu hawa, au nabii, au kuhani watakapokuuliza, ‘Mzigo wa Bwana ni nini?’ wewe utawaambia, ‘Ninyi ndio mzigo. Nami nitawavua kama vazi, asema Bwana.’ 34 agNabii, kuhani, au mtu yeyote akisema, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ nitamwadhibu huyo na nyumba yake. 35 ahHivyo mnaambiana kila mmoja na mwenzake, au kwa mtu wa nyumba yao: ‘Bwana amejibu nini?’ au ‘Bwana amesema nini?’ 36 aiLakini kamwe msiseme tena, ‘Nina mzigo wa Bwana,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe, na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai, Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wetu. 37Hivi ndivyo utakavyoendelea kumuuliza nabii: ‘Bwana amekujibu nini?’ au ‘Je, Bwana amesema nini?’ 38Ingawa unadai, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ hili ndilo Bwana asemalo: Ulitumia maneno, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ hata ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni mzigo wa Bwana.’ 39 ajKwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutupa mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu. 40 akNitaleta juu yako fedheha ya kudumu: yaani aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”

Copyright information for SwhNEN