Jeremiah 3

Israeli Asiye Mwaminifu

1“Kama mtu akimpa talaka mkewe,
naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine,
je, huyo mume aweza kumrudia tena?
Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa?
Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi:
je, sasa utanirudia tena?”
asema BWANA.

2“Inua macho utazame miinuko iliyo kame na uone.
Je, pana mahali ambapo hawajalala nawe?
Uliketi kando ya barabara ukiwasubiri wapenzi,
ukakaa kama yeye ahamahamaye jangwani.
Umeinajisi nchi
kwa ukahaba wako na uovu wako.
3Kwa hiyo mvua imezuiliwa,
wala mvua za vuli hazikunyesha.
Hata hivyo, una uso wa shaba kama wa kahaba;
unakataa kutahayari kwa aibu.
4Je, wewe hujaniita hivi punde tu:
‘Baba yangu, rafiki yangu tangu ujana wangu,
5je, utakasirika siku zote?
Je, ghadhabu yako itaendelea milele?’
Hivi ndivyo unavyozungumza,
lakini unafanya maovu yote uwezayo.”

Wito Kwa Ajili Ya Toba

6Wakati wa utawala wa Mfalme Yosia, BWANA aliniambia, “Umeona kile ambacho Israeli asiyemwaminifu alichofanya? Amepanda juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda na amefanya uzinzi huko. 7Mimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya yote haya angelinirudia lakini hakurudi, naye dada yake Yuda asiye mwaminifu aliona hili. 8Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka na kumfukuza kwa ajili ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake asiyemwaminifu hakuogopa, pia alitoka na kufanya uzinzi. 9Kwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake aliinajisi nchi kwa kuzini na jiwe na mti. 10Pamoja na hayo yote, Yuda dada yake ambaye si mwaminifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asema BWANA.

11BWANA akaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda aliye mdanganyifu. 12Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini: “ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema BWANA,
‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,
kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema BWANA,
‘Sitashika hasira yangu milele.
13Ungama dhambi zako tu:
kwamba umemwasi BWANA Mungu wako,
umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni
chini ya kila mti unaotanda,
nawe hukunitii mimi,’ ”
asema BWANA.14“Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema BWANA. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni. 15Kisha nitawapeni wachungaji wanipendezao moyo wangu ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu. 16Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena ‘Sanduku la Agano la BWANA,’ ” asema BWANA. “Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine. 17Wakati huo, watapaita Yerusalemu kiti cha enzi cha BWANA, nayo mataifa yote watakusanyika Yerusalemu kuliheshimu jina la BWANA. Hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao miovu. 18Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaungana na nyumba ya Israeli, wao kwa pamoja watakuja kutoka nchi ya kaskazini kwenda kwenye nchi niliyowapa baba zenu kama urithi.

19“Mimi mwenyewe nilisema, “ ‘Tazama jinsi nitakavyowatunza kwa furaha kama wana
na kuwapa nchi nzuri,
urithi ulio mzuri kuliko wa taifa jingine lo lote.’
Nilidhani mngeniita ‘Baba’
na kwamba msingegeuka, mkaacha kunifuata.
20Lakini kama mwanamke asiye mwaminifu kwa mumewe,
vivyo hivyo mmekosa uaminifu kwangu pia, Ee nyumba ya Israeli,”
asema BWANA.

21Kilio kinasikika juu ya miinuko iliyo kame,
kulia na kuomboleza kwa watu wa Israeli,
kwa sababu wamepotoka katika njia zao
na wamemsahau BWANA Mungu wao.
22“Rudini, enyi watu msio waaminifu,
nami nitawaponya ukengeufu wenu.”
“Naam, tutakujia
kwa maana wewe ni BWANA Mungu wetu.
23Hakika zile ghasia za kuabudu sanamu kwenye vilima
na milimani ni udanganyifu;
hakika katika BWANA, Mungu wetu,
uko wokovu wa Israeli.
24Tangu ujana wetu miungu ya aibu imeyala
matunda ya kazi za baba zetu:
makundi yao ya kondoo na mbuzi, pamoja na ng'ombe,
wana wao na binti zao.
25Sisi na tulale chini katika aibu yetu,
fedheha yetu na itufunike.
Tumetenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wetu,
sisi na mababa zetu;
tangu ujana wetu hadi leo
hatukumtii BWANA Mungu wetu.”


Copyright information for Neno