Jeremiah 42

Yeremia Ashauri Walionusurika Wasihame Yuda

1 aNdipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia 2 bYeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe Bwana Mungu wako kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu. 3 cOmba ili Bwana Mungu wako atuambie twende wapi na tufanye nini.”

4 dNabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba Bwana Mungu wenu kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho Bwana, wala sitawaficha chochote.”

5 eKisha wakamwambia Yeremia, “Bwana na awe shahidi wa kweli na mwaminifu kati yetu kama hatutafanya sawasawa na kila kitu Bwana Mungu wako atakachokutuma utuambie. 6 fLikiwa jema au likiwa baya, tutamtii Bwana Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii Bwana Mungu wetu.”

7Baada ya siku kumi, neno la Bwana likamjia Yeremia. 8 gKwa hiyo akawaita pamoja Yohanani mwana wa Karea, na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana. 9Akawaambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu: 10 h‘Kama mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo. 11 iMsimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema Bwana, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mikononi mwake. 12 jNitawaonea huruma ili naye awe na huruma nanyi na kuwarudisha katika nchi yenu.’

13 k“Hata hivyo, kama mkisema, ‘Hatutakaa katika nchi hii,’ hivyo mkaacha kumtii Bwana Mungu wenu, 14 lnanyi kama mkisema, ‘Hapana, tutakwenda kuishi Misri, mahali ambapo hatutaona vita au kusikia sauti ya tarumbeta au kuwa na njaa ya chakula,’ 15basi sikieni neno la Bwana, enyi mabaki ya Yuda. Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Ikiwa mmekusudia kwenda Misri na kufanya makazi huko, 16 mbasi ule upanga mnaouogopa utawapata huko, na njaa mnayoihofia itawafuata huko Misri, nanyi mtafia huko. 17 nNaam, wote waliokusudia kwenda kuishi Misri watakufa kwa upanga, njaa na tauni; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika au kuokoka maafa nitakayoyaleta juu yao.’ 18 oHili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyomwagwa juu ya wale walioishi Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu mtakapokwenda Misri. Mtakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha kulaumia na cha kushutumia, nanyi kamwe hamtaona mahali hapa tena.’

19 p“Enyi mabaki ya Yuda, Bwana amewaambia, ‘Msiende Misri.’ Hakikisheni jambo hili: Ninawaonya leo 20 qkwamba mmefanya kosa kubwa mioyoni mwenu mliponituma kwa Bwana Mungu wenu na kusema, ‘Mwombe Bwana Mungu wetu kwa ajili yetu, nawe utuambie kila kitu atakachosema, nasi tutafanya.’ 21 rNimewaambieni leo, lakini bado ninyi hamtaki kumtii Bwana Mungu wenu katika yote aliyonituma niwaambie. 22 sBasi sasa, hakikisheni jambo hili: Mtakufa kwa upanga, njaa na tauni mahali ambapo mnataka kwenda kuishi.”

Copyright information for SwhNEN