Jeremiah 48

Ujumbe Kuhusu Moabu

1Kuhusu Moabu:Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Ole wa Nebo, kwa maana utaharibiwa.
Kiriathaimu utaaibishwa na kutekwa;
Misgabu itaaibishwa na kuvunjwa vunjwa.
2Moabu haitasifiwa tena;
huko Heshboni watu watafanya shauri baya la anguko lake:
‘Njoni na tuangamize taifa lile.’
Wewe nawe, Ee Madmeni, utanyamazishwa;
upanga utakufuatia.
3Sikiliza kilio kutoka Horonaimu,
kilio cha maangamizi makuu na uharibifu.
4Moabu utavunjwa,
wadogo wake watapiga kelele.
5Wanapanda kwenda njia ya kuelekea Luhithi,
wakilia kwa uchungu wanapotembea,
kwenye njia inayoshuka kwenda Horonaimu
kilio cha uchungu kwa ajili ya uharibifu kinasikika.
6Kimbieni! Okoeni maisha yenu,
iweni kama kichaka jangwani.
7Kwa kuwa mmetumainia matendo yenu na mali zenu,
ninyi pia mtachukuliwa mateka,
naye Kemoshi
48.7 Kemoshi alikuwa mungu wa Wamoabu
atakwenda uhamishoni,
pamoja na makuhani wake na maafisa wake.
8Mharabu atakuja dhidi ya kila mji,
wala hakuna mji utakaookoka.
Bonde litaangamizwa na uwanda utaharibiwa,
kwa sababu BWANA amesema.
9Wekeni chumvi kwa ajili ya Moabu,
kwa kuwa ataangamizwa;
miji yake itakuwa ukiwa,
pasipo kuwa na mtu atakayeishi ndani yake.
10“Alaaniwe yeye afanyaye kazi ya BWANA kwa hila!
Alaaniwe yeye auzuiaye upanga wake usimwage damu!
11“Moabu amestarehe tangu ujana wake,
kama divai iliyoachwa kwenye machujo yake,
haikumiminwa kutoka chombo kimoja hadi kingine,
hajaenda uhamishoni.
Kwa hiyo ana ladha ile ile kama aliyokuwa nayo,
nayo harufu yake haijabadilika.
12Lakini siku zinakuja,”
asema BWANA,
“nitakapotuma watu wamiminao kutoka kwenye magudulia,
nao watammimina;
wataacha magudulia yake yakiwa matupu
na kuvunja mitungi yake.
13Kisha Moabu atamwonea aibu mungu wao Kemoshi,
kama vile nyumba ya Israeli walivyoona aibu
wakati walipotegemea mungu wa Betheli
48.13 Betheli ina maana ya Nyumba ya Mungu; lakini pia ni mahali ambapo Mfalme Yeroboamu alisimamisha moja ya sanamu za ndama ili kuabudiwa; nyingine aliiweka huko Dani (1 Fal 12:29-33)
.
14“Mwawezaje kusema, ‘Sisi ni mashujaa,
watu jasiri katika vita’?
15Moabu ataangamizwa na miji yake itavamiwa,
vijana wake waume walio bora sana watachinjwa,”
asema Mfalme, ambaye jina lake
ni BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote.
16“Kuanguka kwa Moabu kumekaribia,
janga kubwa litamjia kwa haraka.
17Ombolezeni kwa ajili yake, ninyi nyote mnaoishi kumzunguka,
ninyi nyote mnaojua sifa zake,
semeni, ‘Tazama jinsi ilivyovunjika fimbo ya kifalme yenye nguvu,
tazama jinsi ilivyovunjika fimbo iliyotukuka!’
18“Shuka kutoka katika fahari yako
na uketi katika ardhi iliyokauka,
Enyi wenyeji wa Binti wa Diboni,
kwa maana yeye aangamizaye Moabu atakuja dhidi yako
na kuangamiza miji yako
iliyozungushiwa maboma.
19Simama kando ya barabara na utazame,
wewe ambaye unaishi Aroeri.
Mwulize mwanaume anayekimbia
na mwanamke anayetoroka,
waulize, ‘Kumetokea nini?’
20Moabu amefedheheshwa, kwa kuwa amevunjwavunjwa.
Lieni kwa huzuni na kupiga kelele!
Tangazeni kando ya Arnoni
kwamba Moabu ameangamizwa.
21Hukumu imefika kwenye uwanda wa juu:
katika Holoni, Yasa na Mefaathi,
22katika Diboni, Nebo
na Beth-Diblathaimu,
23katika Kiriathaimu, Beth-Gamuli
na Beth-Meoni,
24katika Keriothi na Bosra;
kwa miji yote ya Moabu,
iliyoko mbali na karibu.
25Pembe
48.25 Pembe hapa ni ishara ya nguvu
ya Moabu imekatwa,
mkono wake umevunjwa,”
asema BWANA.

26“Mlevye,
kwa kuwa amemdharau BWANA.
Moabu na agaegae katika matapishi yake,
yeye na awe kitu cha dhihaka.
27Je, Israeli hakuwa kitu chako cha kudhihakiwa?
Je, alikamatwa miongoni mwa wezi,
kiasi cha kutikisa kichwa chako kwa dharau
kila mara unapozungumza juu yake?
28Ondokeni kwenye miji yenu na mkaishi katikati ya miamba,
enyi mnaoishi Moabu.
Iweni kama huwa ambaye hutengeneza kiota
chake kwenye mdomo wa pango.
29“Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu:
kutakabari kwake kwa kiburi na majivuno,
kiburi chake na ufidhuli wake,
na kujivuna kwa moyo wake.
30Ninaujua ujeuri wake lakini ni bure,”
asema BWANA,

“nako kujisifu kwake hakumsaidii cho chote.
31Kwa hiyo namlilia Moabu,
kwa ajili ya Moabu yote ninalia,
ninaomboleza kwa ajili
ya watu wa Kir-Haresethi.
32Ninalia machozi kwa ajili yenu,
kama Yazeri aliavyo,
Enyi mizabibu ya Sibma.
Matawi yako yameenea mpaka baharini;
yamefika mpaka Bahari ya Yazeri.
Mwarabu ameanguka juu ya matunda yako
yaliyoiva na mizabibu.
33Shangwe na furaha vimetoweka
kutoka kwenye bustani na mashamba ya Moabu.
Nimekomesha kutiririka kwa divai kutoka katika mashinikizo;
hakuna hata mmoja ayakanyagaye
kwa kelele za shangwe.
Ingawa kuna kelele,
sio za shangwe.
34“Sauti ya kilio chao inapanda
kutoka Heshboni mpaka Eleale na Yahazi,
kutoka Soari mpaka Horonaimu na Eglath-Shelishiya,
kwa kuwa hata maji ya Nimrimu yamekauka.
35Katika Moabu nitakomesha wale wote watoao sadaka
mahali pa juu pa kuabudia miungu,
na kufukiza uvumba kwa miungu yao,”
asema BWANA.

36“Kwa hiyo moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama filimbi;
unaomboleza kama filimbi
kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.
Utajiri waliojipatia umetoweka.
37Kila kichwa kimenyolewa
na kila mwenye ndevu zimekatwa;
kila mkono umekatwa na kila kiuno kimefunikwa
kwa nguo ya gunia.
38Juu ya mapaa yote katika Moabu
na katika viwanja
hakuna kitu cho chote isipokuwa maombolezo,
kwa kuwa nimemvunja Moabu
kama gudulia ambalo hakuna mtu ye yote anayelitaka,”
asema BWANA.

39“Tazama jinsi alivyovunjikavunjika!
Jinsi wanavyolia kwa huzuni!
Tazama jinsi Moabu anavyogeuka kwa aibu!
Moabu amekuwa kitu cha kudhihakiwa,
kitu cha kutisha kwa wale wote
wanaomzunguka.”40Hili ndilo asemalo BWANA: “Tazama! Tai anashuka chini,
akitanda mbawa zake juu ya Moabu.
41Miji itatekwa na ngome zake
zitatwaliwa.
Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Moabu
itakuwa kama moyo wa mwanamke
aliye katika utungu wa kuzaa.
42Moabu ataangamizwa kama taifa
kwa sababu amemdharau BWANA.
43Hofu kuu, shimo na mtego unawangojea,
Enyi watu wa Moabu,”
asema BWANA.

44“Ye yote atakayeikimbia hiyo hofu kuu
ataanguka ndani ya shimo,
ye yote atakayepanda kutoka shimoni,
atanaswa katika mtego,
kwa sababu nitaleta juu ya Moabu
mwaka wa adhabu yake,”
asema BWANA.

45“Katika kivuli cha Heshboni,
wakimbizi wamesimama pasipo msaada,
kwa kuwa moto umezimika huko Heshboni,
mwali wa moto kutoka katikati ya Sihoni;
unaunguza vipaji vya nyuso za Moabu,
mafuvu yao wenye kujivuna kwa kelele.
46Ole wako, Ee Moabu!
Watu wa Kemoshi wameangamizwa;
wana wako wamepelekwa uhamishoni
na binti zako wamechukuliwa mateka.
47“Lakini nitarudisha mateka wa Moabu,
katika siku zijazo,”
asema BWANA.Huu ndio mwisho wa hukumu juu ya Moabu.

Copyright information for Neno