Jeremiah 5

Hakuna Hata Mmoja Aliye Mkamilifu

1“Pandeni na kushuka katika mitaa ya Yerusalemu,
tazameni pande zote na mkumbuke,
tafuteni katika viwanja vyake.
Kama mtaweza kumpata hata mtu mmoja tu
atendaye kwa uaminifu na kutafuta kweli,
nitausamehe mji huu.
2Ingawa wanasema, ‘Kwa hakika kama BWANA aishivyo,’
bado wanaapa kwa uongo.”
3Ee BWANA, je, macho yako hayaitafuti kweli?
Uliwapiga, lakini hawakusikia maumivu,
uliwapondaponda lakini walikataa marudi.
Walifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko jiwe
nao walikataa kutubu.
4Ndipo nikasema, “Hawa ni maskini tu;
wao ni wapumbavu,
kwa maana hawaijui njia ya BWANA,
sheria ya Mungu wao.
5Kwa hiyo nitakwenda kwa viongozi
na kuzungumza nao,
hakika wao wanaijua njia ya BWANA,
sheria ya Mungu wao.”
Lakini kwa nia moja nao pia walikuwa wameivunja nira
na kuvivunja vifungo.
6Kwa hiyo simba kutoka mwituni atawashambulia,
mbwa mwitu kutoka jangwani atawaangamiza,
chui atawavizia karibu na miji yao
kumrarua vipande vipande ye yote
atakayethubutu kutoka nje,
kwa maana maasi yao ni makubwa
na kukengeuka kwao kumekuwa ni kwingi.
7“Kwa nini niwasamehe?
Watoto wenu wameniacha
na kuapa kwa miungu ambayo si miungu.
Niliwapatia mahitaji yao yote,
lakini bado wamefanya uzinzi
na kusongana katika nyumba za makahaba.
8Wamelishwa vizuri, kama farasi waume wenye tamaa nyingi,
kila mmoja akimlilia
mke wa mwanaume mwingine.
9Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?”
asema BWANA.
“Je, nisijilipizie kisasi
juu ya taifa kama hili?
10“Piteni katika mashamba yake ya mizabibu na kuyaharibu,
lakini msiangamize kabisa.
Pogoeni matawi yake,
kwa kuwa watu hawa sio wa BWANA.
11Nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda
wamekuwa si waaminifu kwangu kamwe,”
asema BWANA.

12Wamedanganya kuhusu BWANA,
wamesema, “Yeye hatafanya jambo lo lote!
Hakuna dhara litakalotupata;
kamwe hatutaona upanga wala njaa.
13Manabii ni upepo tu, wala neno halimo ndani yao,
kwa hiyo hayo wayasemayo
na yatendeke kwao.”
14

Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote: “Kwa sababu watu hawa wamesema maneno haya,
nitayafanya maneno yangu
vinywani mwenu kuwa moto
na watu hawa wawe kuni
zinazoliwa na huo moto.
15Ee nyumba ya Israeli,” asema BWANA,
“Ninaleta taifa toka mbali dhidi yako,
taifa la kale na linaloendelea kudumu,
taifa ambalo lugha yao huijui,
wala msemo wao huwezi kuuelewa.
16Podo zao ni kama kaburi lililo wazi,
wote ni mashujaa hodari wa vita.
17Watayaangamiza mazao yenu na chakula chenu,
wataangamiza wana wenu na mabinti zenu;
wataangamiza makundi yenu
ya kondoo na mbuzi, na ya ng'ombe,
wataangamiza mizabibu yenu na mitini yenu.
Kwa upanga wataangamiza
miji yenye maboma mliyoitumainia.18“Hata hivyo katika siku hizo, sitakuangamiza kabisa,” asema BWANA. 19“Nao watu watakapouliza, ‘Kwa nini BWANA, Mungu wetu ametufanyia mambo haya yote?’ Utawaambia, ‘Kama vile mlivyoniacha mimi na kutumikia miungu migeni katika nchi yenu wenyewe, ndivyo sasa mtakavyowatumikia wageni katika nchi ambayo si yenu.’ 20“Itangazie nyumba ya Yakobo hili
na ulipigie mbiu katika Yuda:
21Sikieni hili, enyi wapumbavu na watu msio na akili,
mlio na macho lakini hamwoni,
mlio na masikio lakini hamsikii:
22Je, haiwapasi kuniogopa mimi?” asema BWANA.
“Je, haiwapasi kutetemeka mbele zangu?
Niliufanya mchanga kuwa mpaka wa bahari,
kizuizi cha milele ambacho haiwezi kupita.
Mawimbi yanaweza kuumuka, lakini hayawezi kuupita;
yanaweza kunguruma, lakini hayawezi kuuvuka.
23Lakini watu hawa wana mioyo ya ukaidi na ya uasi,
wamegeukia mbali na kwenda zao.
24Wao hawaambiani wenyewe,
‘Sisi na tumwogope BWANA Mungu wetu,
anayetupatia mvua za masika na za vuli
kwa majira yake,
anayetuhakikishia majuma ya mavuno
kwa utaratibu.’
25Matendo yenu mabaya yamezuia haya yote,
dhambi zenu zimewafanya msipate mema.
26“Miongoni mwa watu wangu wamo walio waovu
wanaovizia kama watu wanaotega ndege
na kama wale wanaoweka mitego
kuwakamata watu.
27Kama vitundu vilivyojaa ndege,
nyumba zao zimejaa udanganyifu;
wamekuwa matajiri na wenye nguvu,
28wamenenepa na kunawiri.
Matendo yao maovu hayana kikomo;
hawatetei mashauri ya yatima
wapate kushinda,
hawatetei haki za maskini.
29Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?”
asema BWANA.
“Je, nisijilipizie kisasi
juu ya taifa kama hili?
30“Jambo la kutisha na kushtusha
limetokea katika nchi hii:
31Manabii wanatabiri uongo,
makuhani wanatawala
kwa mamlaka yao wenyewe,
nao watu wangu wanapenda hivyo.
Lakini mtafanya nini mwisho wake?


Copyright information for Neno