Jeremiah 9

1Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji
na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!
Ningelia mchana na usiku
kwa kuuawa kwa watu wangu.
2Laiti ningekuwa na nyumba
ya kukaa wasafiri katika jangwa,
ningewaacha watu wangu
na kwenda mbali nao,
kwa kuwa wote ni wazinzi,
kundi la watu wasio waaminifu.
3“Huweka tayari ndimi zao kama upinde,
ili kurusha uongo;
wamekuwa na nguvu katika nchi
kwa ajili ya uongo,
wala si katika kweli.
Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,
hawanitambui mimi,”
asema BWANA.

4“Jihadhari na rafiki zako;
usiwaamini ndugu zako.
Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,
na kila rafiki ni msingiziaji.
5Rafiki humdanganya rafiki,
hakuna ye yote asemaye kweli.
Wamefundisha ndimi zao kudanganya,
wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.
6Unakaa katikati ya udanganyifu;
katika udanganyifu wao
wanakataa kunitambua mimi,”
asema BWANA.

7

Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,
kwani ni nini kingine niwezacho kufanya
kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?
8Ndimi zao ni mshale wenye sumu,
hunena kwa udanganyifu.
Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,
lakini moyoni mwake humtegea mtego.
9Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”
Asema BWANA.
“Je, nisijilipizie kisasi
kwa taifa kama hili?”
10Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.
Yamekuwa ukiwa na wala hakuna apitaye humo,
milio ya ng'ombe haisikiki.
Ndege wa angani wameruka
na wanyama wameondoka.
11“Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,
makao ya mbweha;
nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa
ili asiwepo atakayeishi humo.”12Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na BWANA awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?

13BWANA akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu. 14Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata mabaali, kama vile baba zao walivyowafundisha.” 15Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu. 16Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao hawakuwajua wala baba zao, nitawafuatia kwa upanga mpaka niwe nimewaangamiza kabisa.”17Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezao waje,
waite wale walio na ustadi kuliko wote.
18Nao waje upesi
kutuombolezea
mpaka macho yetu yafurike machozi
na vijito vya maji vitoke kwenye kope zetu.
19Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:
‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!
Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!
Ni lazima tuihame nchi yetu
kwa sababu nyumba zetu
zimekuwa magofu.’ ”
20Basi, enyi wanawake, sikieni neno la BWANA;
fungueni masikio yenu
msikie maneno ya kinywa chake.
Wafundisheni binti zenu jinsi ya kuomboleza;
fundishaneni kila mmoja na mwenzake kuomboleza.
21Mauti imeingia ndani kupitia madirishani
na imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;
imewakatilia mbali watoto katika barabara
na vijana waume kutoka katika viwanja vya miji.22Sema, “Hili ndilo asemalo BWANA: “ ‘Maiti za wanaume zitalala
kama mavi katika mashamba,
kama malundo ya nafaka yaliyokatwa
yalalavyo nyuma ya mvunaji,
wala hakuna anayekusanya.’ ”23Hili ndilo asemalo BWANA: “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake
au mwenye nguvu asijisifu katika nguvu zake
au tajiri asijisifu katika utajiri wake,
24lakini yeye ajisifuye na ajisifu kwa sababu hili:
kwamba ananifahamu na kunijua mimi,
kwamba mimi ndimi BWANA, nitendaye wema,
hukumu na haki duniani,
kwa kuwa napendezwa na haya,”
asema BWANA.25“Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema BWANA, 26yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

Copyright information for Neno