Job 1

SEHEMU YA KWANZA: HABARI ZA AWALI

Ayubu Na Jamaa Yake

1Katika nchi ya Usi paliishi mtu ambaye jina lake aliitwa Ayubu. Mtu huyu alikuwa hana hatia, naye alikuwa mkamilifu, alimcha Mungu na kuepuka ubaya. 2Alikuwa na wana saba na binti watatu, 3naye alikuwa na kondoo 7,000, ngamia 3,000, jozi 500 za maksai, punda 500, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu mkuu sana miongoni mwa watu wa Mashariki.

4Wanawe walikuwa na desturi ya kufanya karamu katika nyumba zao kwa zamu, nao wangewaalika ndugu zao watatu ili kula na kunywa pamoja nao. 5Wakati kipindi cha karamu kimemalizika, Ayubu angetuma waitwe na kuwafanyia utakaso. Angetoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao asubuhi na mapema, akifikiri, “Pengine wanangu wametenda dhambi na kumlaani Mungu mioyoni mwao.” Hii ilikuwa ndiyo desturi ya kawaida ya Ayubu.

Jaribu La Kwanza La Ayubu

6Siku moja wana wa Mungu
1.6 Wana wa Mungu hapa ina maana malaika au viumbe vya mbinguni
walikwenda kujionyesha mbele za BWANA. Shetani
1.6 Shetani hapa ina maana ya Mshitaki wa watakatifu
naye akaja pamoja nao.
7BWANA akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”

Shetani akamjibu BWANA, “Natoka kuzunguka pote duniani, nikitembea huku na huko humo.”

8Ndipo BWANA akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Mtu ambaye hakuna mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.”

9Shetani akajibu, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? 10Je, wewe hukumjengea boma pande zote yeye na wa nyumbani mwake pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. 11Lakini nyosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”

12BWANA akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, kila kitu alicho nacho kiko mikononi mwako, lakini juu ya huyo mtu mwenyewe usimguse hata kwa kidole.”

Ndipo Shetani akatoka mbele za BWANA.

13Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 14akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, 15Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”

16Wakati alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”

17Wakati alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari.”

18Wakati alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako na binti zako walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 19ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”

20Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akaanguka chini katika kuabudu 21na kusema: “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi,
nami nitaondoka uchi
1.21 Au: nitarudi huko uchi
,
BWANA alinipa, naye BWANA ameviondoa,
jina la BWANA litukuzwe.”22Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi, wala kumlaumu Mungu kwa kufanya ubaya.

Copyright information for Neno