Job 11

Sofari Anasema: Hatia Ya Ayubu Inastahili Adhabu

1Ndipo Sofari, Mnaamathi akajibu: 2“Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa?
Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?
3Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya?
Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?
4Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili
nami ni safi mbele zako.’
5Aha! Laiti kwamba Mungu angesema,
kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,
6naye akufunulie siri za hekima,
kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili.
Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.
7“Je, waweza kujua siri za Mungu?
Je, waweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?
8Ni juu mno kuliko mbingu: waweza kufanya nini?
Kina chake ni kirefu kuliko kuzimu:
wewe waweza kujua nini?
9Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia
nacho ni kipana kuliko bahari.
10“Kama akija na kukufunga gerezani
na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?
11Hakika anawatambua watu wadanganyifu,
naye aonapo uovu, je, haangalii?
12Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima,
endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.
13“Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake
na kumwinulia mikono yako,
14ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako
wala usiuruhusu uovu ukae hemani mwako,
15ndipo utainua uso wako bila aibu,
utasimama imara bila hofu.
16Hakika utaisahau taabu yako,
utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.
17Maisha yako yatang'aa kuliko adhuhuri,
nalo giza litakuwa kama alfajiri.
18Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini;
utatazama kukuzunguka pande zote
na kupumzika kwa salama.
19Utalala, wala hakuna atakayekuogofya,
naam, wengi watajipendekeza kwako ili kupata fadhili.
20Bali macho ya waovu hayataona,
wokovu utawaepuka;
tarajio lao litakuwa ni hangaiko
la mtu anayekata roho.”


Copyright information for Neno