Job 13

“Macho yangu yameona hili lote,
masikio yangu yamesikia na kulielewa.
Hayo mnayoyajua mimi pia ninayajua,
mimi si mtu duni kuliko ninyi.
Lakini ninayo shauku ya kuzungumza na Mwenyezi
na kuhojiana shauri langu na Mungu.
Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo,
ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!
Laiti wote mngenyamaza kimya!
Kwa kuwa kwenu hilo lingekuwa hekima.
Sikieni sasa hoja yangu,
mkasikilize kusihi kwangu.
Je, mtazungumza kwa uovu kwa niaba ya Mungu?
Je, mtazungumza kwa udanganyifu kwa niaba yake?
Mtamwonyesha upendeleo?
Mtamtetea Mungu kwenye mashtaka yake?
Je, ingekuwa vyema Mungu akiwahoji ninyi?
Je, mngeweza kumdanganya kama ambavyo mngeweza kuwadanganya wanadamu?
10 Hakika angewakemea
kama mkiwapendelea watu kwa siri.
11 Je, huo ukuu wake haungewatisha ninyi?
Je, hofu yake isingewaangukia ninyi?
12 Maneno yenu ni mithali za majivu;
utetezi wenu ni ngome za udongo wa mfinyanzi.
13 “Nyamazeni kimya nipate kusema,
kisha na yanipate yatakayonipata.
14 Kwa nini nijiweke mwenyewe kwenye hatari
na kuyaweka maisha yangu mikononi mwangu?
15 Ingawa ataniua, bado nitamtumaini;
hakika nitazitetea njia zangu mbele zake.
16 Naam, hili litanigeukia kuwa wokovu wangu,
kwa maana hakuna mtu asiyemcha Mungu
atakayethubutu kuja mbele yake!
17 Sikilizeni maneno yangu kwa makini,
nayo masikio yenu yaingize kile nisemacho.
18 Sasa kwamba nimekwisha kutayarisha mambo yangu,
ninajua mimi nitahesabiwa kuwa na haki.
19 Je, kuna ye yote anayeweza kuleta mashtaka dhidi yangu?
Kama ndivyo, nitanyamaza kimya na nife.
20 “Ee Mungu, unijalie tu mimi haya mambo mawili,
nami sitajificha uso wako:
21 Ondoa mkono wako uwe mbali nami,
nawe uache kuniogofya kwa hofu zako kuu.
22 Niite kwenye shauri nami nitajibu,
au niache niseme, nawe upate kujibu.
23 Ni makosa na dhambi ngapi nilizotenda?
Nionyeshe kosa langu na dhambi yangu.
24 Kwa nini kuuficha uso wako
na kunihesabu mimi kuwa adui yako?
25 Je, utaliadhibu jani lipeperushwalo na upepo?
Je, utayasaka makapi makavu?
26 Kwa kuwa unaandika mambo machungu dhidi yangu
na kunifanya nizirithi dhambi za ujana wangu.
27 Umeifunga miguu yangu kwenye pingu,
na kuzichunga kwa makini njia zangu zote
kwa kutia alama kwenye nyayo za miguu yangu.
28 “Hivyo mwanadamu huangamia
kama kitu kilichooza,
mfano wa vazi lililoliwa na nondo.
Copyright information for Neno