Job 29

Ayubu Anamaliza Utetezi wake

1Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema: 2“Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita,
zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,
3wakati taa yake iliponiangazia juu ya kichwa changu
na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza!
4Aha! Katika siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu,
wakati urafiki wa Mungu wa ndani
ulipoibariki nyumba yangu,
5wakati Mwenyezi alipokuwa pamoja nami,
nao watoto wangu walipokuwa wamenizunguka,
6wakati njia yangu ilipokuwa imenyweshewa siagi,
nao mwamba uliponimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.
7“Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji
na kuketi katika kiwanja,
8vijana waliniona wakakaa kando,
nao wazee walioketi wakasimama,
9wakuu wakaacha kuzungumza
na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao,
10wenye vyeo wakanyamazishwa,
nazo ndimi zao zikagandamana
na makaakaa ya vinywa vyao.
11Ye yote aliyenisikia alinena mema juu yangu,
nao wale walioniona walinisifu,
12kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada,
naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.
13Mtu aliyekuwa karibu na kufa alinibariki,
nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.
14Niliivaa haki kama vazi langu,
uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.
15Nilikuwa macho ya kipofu
na miguu kwa kiwete.
16Nilikuwa baba kwa mhitaji,
nilimtetea mgeni.
17Niliyavunja meno makali ya waovu
na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.
18“Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe,
nazo siku zangu zitakuwa nyingi
kama chembechembe za mchanga.
19Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji,
nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.
20Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu,
upinde wangu daima utaendelea
kuwa mpya mkononi mwangu.’
21“Watu walinisikiliza kwa tumaini,
wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.
22Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi,
maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.
23Waliningojea kama manyunyu ya mvua
na kuyapokea maneno yangu
kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.
24Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha,
nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.
25Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao;
niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake;
nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.


Copyright information for Neno