Job 30

1“Lakini sasa watu wadogo kwa umri
kuliko mimi wananidhihaki,
watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau
kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.
2Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu,
kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
3Kukonda kwao kutokana na kupungukiwa na kwa njaa,
walizungukazunguka usiku katika nchi kame iliyo ukiwa,
isiyolimika wala kukaliwa na watu
4Katika vichaka walikusanya mimea yenye ladha ya chumvi,
nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.
5Walifukuzwa mbali na watu wao,
wakipigiwa kelele kama wevi.
6Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka,
kwenye majabali na mahandaki.
7Kwenye vichaka walilia kama punda
na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.
8Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya,
waliofukuzwa watoke katika nchi.
9“Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo,
nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
10Wananichukia sana na kujitenga nami,
wala hawasiti kunitemea mate usoni.
11Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza
kamba ya upinde wangu na kunitesa,
wamekuwa huru kunitendea waonavyo.
12Kuume kwangu kundi linashambulia;
huitegea miguu yangu tanzi,
hunizunguka kwa vita
wakiruka huko na huko kwa ukali dhidi yangu.
13Huizuia njia yangu,
nao hufanikiwa katika kuniletea maafa,
nami sina ye yote wa kunisaidia.
14Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana
katika ngome yangu;
katikati ya magofu huja na kunishambulia.
15Vitisho vimenifunika;
heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo,
salama yangu imetoweka kama wingu.
16“Sasa maisha yangu yamefikia mwisho,
siku za mateso zimenikamata.
17Usiku mifupa yangu inachoma,
maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.
18Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo,
hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.
19Yeye amenitupa kwenye matope,
nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.
20“Ee BWANA, ninakulilia wewe lakini hunijibu,
ninasimama, nawe unanitazama tu.
21Wewe unanigeukia bila huruma,
unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.
22Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo,
umenirusha huko na huko kwenye dhoruba kali.
23Ninajua utanileta mpaka kifoni,
mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.
24“Hakika hakuna ye yote amshambuliaye mhitaji,
anapoomba msaada katika shida yake.
25Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?
Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
26Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia,
nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.
27Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii,
siku za mateso zinanikabili.
28Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua,
ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.
29Nimekuwa ndugu wa mbweha,
rafiki wa mabundi.
30Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika,
mifupa yangu inaungua kwa homa.
31Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo,
nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.
Copyright information for Neno