Job 31

1“Nimefanya agano na macho yangu
yasimtazame msichana kwa kumtamani.
2Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni nini
kutoka kwa Mungu juu,
nao urithi wake ni nini
kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu Aliye juu!
3Je, si uharibifu kwa watu waovu,
maangamizi kwa wale watendao mabaya?
4Je, yeye hazioni njia zangu
na kuihesabu kila hatua yangu?
5“Kama nimeishi katika uongo
au mguu wangu umekimbilia udanganyifu,
6Mungu na anipime katika mizani za uaminifu,
naye atajua kwamba sina hatia,
7kama hatua zangu zimepotoka kutoka kwenye njia,
kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu,
au kama mikono yangu imetiwa unajisi,
8basi wengine na wale vile nilivyovipanda,
nayo yale yote niliyootesha na yang'olewe.
9“Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke,
au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu,
10basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine,
nao wanaume wengine walale naye.
11Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu,
naam, dhambi ya kuhukumiwa.
12Ni moto uwakao kwa Uharibifu
31.12 Yaani Kuzimu; kwa Kiebrania ni Abadon ambayo maana yake ni sawa na Sheol (Ayubu 26:6; Mit 15:11)
;
ungekuwa umeng'oa mavuno yangu.
13“Kama ningewanyima haki
watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu,
walipokuwa na nung'uniko dhidi yangu,
14nitafanya nini Mungu atakaponikabili?
Nitamjibu nini nitakapoitwa kutoa hesabu?
15Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu,
si ndiye aliyewaumba?
Je, si yeye huyo mmoja aliyetuumba sote
ndani ya mama zetu?
16“Ikiwa nimewanyima maskini haja zao,
au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike,
17kama nimekula chakula changu mwenyewe,
bila kuwashirikisha yatima;
18lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima
kama ambavyo baba angefanya,
nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane:
19kama nilimwona ye yote akiteseka kwa kukosa nguo,
au mtu mhitaji asiye na mavazi
20ambaye wala moyo wake haukunibariki
kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo zangu
21na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima,
nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani,
22basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu,
nao na uvunjike kutoka katika kiungio chake.
23Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu,
nami kwa kuuogopa utukufu wake
sikuweza kufanya mambo kama hayo.
24“Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu,
au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’
25kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu,
ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,
26kama nimelitazama jua katika kung'aa kwake
au mwezi ukienda kwa fahari yake,
27hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri,
au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,
28basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa,
kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu
kwa Mungu aishiye juu sana.
29“Kama nimeshangilia msiba wa adui yangu,
au kutazama kwa furaha taabu iliyomjia,
30sikuruhusu kinywa changu kufanya dhambi
kwa kuomba laana dhidi ya maisha yake,
31kama watu wa nyumbani mwangu kamwe hawakusema,
‘Ni nani ambaye hajashibishwa na nyama ya Ayubu?’
32Hakuna mgeni aliyelala njiani,
kwa maana mlango wangu ulikuwa wazi kwa msafiri,
33kama nimeifunika dhambi yangu kama wanadamu wengine wafanyavyo,
kwa kuficha hatia yangu moyoni mwangu,
34kwa sababu ya kuogopa umati wa watu
na hivyo kuwa na hofu ya kudharauliwa na jamaa,
nikanyamaza kimya nisitoke nje ya mlango:
35(“Laiti kama angekuwapo mtu wa kunisikia!
Tazama sasa ninatia sahihi kwenye utetezi wangu:
Mwenyezi na anijibu;
mshitaki wangu na aweke mashtaka yake
kwenye maandishi.
36Hakika ningeyavaa begani mwangu,
ningeyavaa kama taji.
37Ningempa hesabu ya kila hatua yangu,
ningemwendea kama mwana wa mfalme):
38“Kama nchi yangu inalia dhidi yangu
na mifereji yake yote imelowana kwa machozi,
39kama nimekula mazao yake bila malipo,
au kuvunja mioyo ya wapangaji wake,
40basi miiba na iote badala ya ngano
na magugu badala ya shayiri.”

Mwisho wa maneno ya Ayubu.

Copyright information for Neno