Job 35

Elihu Analaumu Mtu Kujiona Kuwa Mwenye Haki

Ndipo Elihu akasema: “Je, unadhani hili ni haki?
Wewe unasema, ‘Nina haki mbele za Mungu.’
Bado unamwuliza, ‘Ni faida gani nimepata
na nimefaidi nini kwa kutokutenda dhambi?’
“Ningependa nikujibu wewe
pamoja na marafiki zako walio pamoja nawe.
Tazama juu mbinguni ukaone,
yaangalie mawingu yaliyo juu sana juu yako.
Je, ukitenda dhambi, inamdhuruje Mungu?
Kama dhambi zako zikiwa nyingi,
hilo linamfanyia nini Mungu?
Kama wewe ni mwadilifu, unampa nini,
au yeye anapokea nini mkononi kwako?
Uovu wako unamdhuru tu mtu mwingine kama wewe,
nayo haki yako inawafaa wanadamu tu.
“Wanadamu hulia kwa kulemewa na mateso,
huomba msaada kutoka kwenye mkono wenye nguvu.
10 Lakini hakuna asemaye,
‘Yuko wapi Mungu Muumba wangu,
yeye anifanyaye niimbe usiku,
11 yeye atufundishaye sisi zaidi kuliko wanyama wa dunia,
na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani?’
12 Yeye hajibu wakati watu waliapo
kwa sababu ya kiburi cha watu waovu.
13 Naam, Mungu hasikilizi maombi yao ya ubatili,
Mwenyezi hayazingatii.
14 Si zaidi sana kwamba hatakusikiliza
wewe usemapo humwoni,
tena ya kwamba shauri lako liko mbele zake
na wewe lazima umngojee,
15 pia zaidi, kwamba hasira yake kamwe haiadhibu
wala haangalii uovu hata kidogo?
16 Hivyo Ayubu hufumbua kinywa chake
kwa maneno yasiyo na maana;
anaongea maneno mengi bila maarifa.”


Copyright information for Neno