Job 37

“Kwa hili moyo wangu unatetemeka,
nao unaruka kutoka mahali pake.
Sikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake,
sauti ya ngurumo itokayo kinywani mwake.
Huuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote
na kuupeleka hata miisho ya dunia.
Baada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake,
Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari.
Wakati sauti yake ingurumapo tena,
huuachilia umeme wake wa radi.
Sauti ya Mungu hunguruma kwa jinsi ya ajabu,
hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.
Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’
na huyaambia manyunyu ya mvua,
‘Uwe mvua ya nguvu.’
Ili kwamba wanadamu wote aliowaumba
wapate kujua kazi zake,
humzuilia kila mtu shughuli zake.
Wanyama hujificha;
hubakia kwenye mapango yao.
Dhoruba hutoka katika chumba chake,
baridi hutoka katika upepo uendao kasi.
10 Pumzi ya Mungu hutoa barafu,
eneo kubwa la maji huganda.
11 Huyasheheneza mawingu kwa maji,
naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.
12 Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake,
juu ya uso wa dunia yote,
kufanya lo lote ayaamuruyo.
13 Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu,
au kuinyeshea dunia yake
na kuonyesha upendo wake.
14 “Ayubu, sikiliza hili;
nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.
15 Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu
na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?
16 Je, wajua jinsi mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia,
hayo maajabu yake yeye aliyemkamilifu katika maarifa?
17 Wewe unayeshindwa na joto katika nguo zako
wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini,
18 je, waweza kuungana naye katika kuzitandaza anga,
zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa?
19 “Tuambieni yatupasayo kumwambia,
hatuwezi kutayarisha shauri letu
kwa sababu ya ujinga wetu.
20 Je, aambiwe kwamba nataka kuongea?
Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa?
21 Basi hakuna awezaye kulitazama jua,
kwa jinsi linavyong'aa angani,
upepo ukishafagia mawingu.
22 Kutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu,
Mungu huja katika utukufu wa kutisha.
23 Yeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia, naye ametukuzwa katika uweza;
katika hukumu zake na haki yake kuu, hataonea.
24 Kwa hiyo, wanadamu mheshimuni,
kwa kuwa yeye hamstahi ye yote
anayejidhania kuwa ana hekima.”
Copyright information for Neno