Job 6

Hotuba Ya Pili Ya Ayubu

Ayubu Anajibu: Malalamiko Yangu Ni Ya Haki

1Kisha Ayubu akajibu: 2“Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa,
nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani!
3Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote,
kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.
4Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu,
roho yangu inakunywa sumu yake,
vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.
5Je, punda-mwitu hulia akiwa na majani,
au ng'ombe dume hulia akiwa na chakula?
6Je, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi,
au upo utamu katika ute mweupe wa yai?
7Ninakataa kuvigusa,
vyakula vya aina hii hunichukiza.
8“Laiti ningepata haja yangu,
kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia,
9kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda,
kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali!
10Ndipo bado ningekuwa na hii faraja,
bado ningekuwa na furaha katika maumivu makali:
kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.
11“Ninazo nguvu gani, hata niendelee kutumaini?
Matazamio yangu ya mbele ni nini, hata niendelee kuwa mvumilivu?
12Je, mimi nina nguvu za jiwe?
Je, mwili wangu ni shaba?
13Je, ninao uwezo wo wote wa kujisaidia mimi mwenyewe,
wakati ambapo mafanikio yamefukuziwa mbali nami?
14“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,
hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.
15Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa,
ni kama vijito vya msimu,
ni kama vijito ambavyo hufurika
16wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo
ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,
17lakini hukauka majira ya ukame,
na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.
18Misafara hugeuka kutoka katika njia zake,
hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.
19Misafara ya Tema inatafuta maji,
wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri
hutazama kwa matarajio.
20Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini,
walipofika huko, wakahuzunika
kwa kukosa walichotarajia.
21Sasa nanyi mmethibitika kwamba hamna msaada wo wote,
mnaona jambo la kutisha nanyi mnaogopa.
22Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu,
au mnilipie fidia kutoka katika mali zenu,
23au niokoeni mikononi mwa adui,
au nikomboeni kutoka kwenye makucha
ya wasio na huruma’?
24“Nifundisheni, nami nitanyamaza kimya,
nionyesheni nilikokosea.
25Tazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli!
Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini?
26Je, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema,
na kuyafanya maneno ya mtu
anayekata tamaa kama upepo?
27Mngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima
na kubadilishana rafiki yenu na mali.
28“Lakini sasa iweni na huruma mkaniangalie mimi.
Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu?
29Tulizeni hasira, msiwe wadhalimu;
angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu
6.29 Au: haki yangu bado inasimama
.
30Je, pana uovu wo wote midomoni mwangu?
Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?


Copyright information for Neno