Jonah 3

Yona Aenda Ninawi

1Ndipo neno la BWANA likamjia Yona mara ya pili: 2“Ondoka uende katika mji mkubwa wa Ninawi, ukautangazie ujumbe ninaokupa.”

3Yona akalitii neno la BWANA naye akaenda Ninawi. Basi Ninawi ulikuwa mji maarufu sana, ilichukua siku tatu kuuzunguka. 4Siku ya kwanza, Yona aliingia mjini. Akatangaza: “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.” 5Watu wa Ninawi wakamwamini Mungu, wakatangaza kufunga, watu wote kuanzia mkubwa sana hadi yule mdogo kabisa, wakavaa nguo za gunia.

6Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha enzi, akavua majoho yake ya kifalme, akajifunika nguo ya gunia kisha akaketi chini mavumbini. 7Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote:“Kwa amri ya mfalme na wakuu wake:

“Msiruhusu mtu ye yote au mnyama, makundi ya ng'ombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu cho chote, msiwaruhusu kula wala kunywa.
8Bali wanadamu na wanyama wafunikwe kwa nguo za gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao. 9Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie.”10Mungu alipoona walivyofanya na jinsi walivyogeuka kutoka katika njia zao mbaya, akawa na huruma wala hakuleta maangamizi juu yao kama alivyokuwa ameonya.

Copyright information for Neno