Joshua 1

BWANA Anamwagiza Yoshua

1Baada ya kifo cha Mose mtumishi wa BWANA, BWANA akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Mose: 2“Mtumishi wangu Mose amekufa. Sasa basi, wewe pamoja na watu wote hawa, jiandaeni kuvuka huu Mto Yordani kuingia nchi ambayo karibu nitawapa wana wa Israeli. 3Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Mose. 4Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto huu mkubwa wa Eufrati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa
1:4 Yaani Bahari ya Mediterania
iliyoko upande wa magharibi.
5Hakuna mtu ye yote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.

6“Uwe hodari na moyo wa ushujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7Uwe hodari tu na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria zote alizokupa Mose mtumishi wangu, usiziache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa po pote uendako. 8Usiache Kitabu hiki cha Torati kiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapoifanikisha njia yako na kisha utastawi sana. 9Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe imara na hodari sana. Usiogope wala usivunjike moyo, kwa kuwa BWANA Mungu wako atakuwa pamoja nawe ko kote uendako.”

10Ndipo Yoshua akawaagiza viongozi wa watu akisema, 11“Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Wekeni tayari mahitaji yenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka hii Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo BWANA Mungu wenu anawapa iwe yenu wenyewe.’ ”

12Lakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema, 13“Kumbukeni agizo lile Mose mtumishi wa BWANA alilowapa: ‘BWANA Mungu wenu anawapa ninyi raha, naye amewapa nchi hii.’ 14Wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ile Mose aliyowapa mashariki ya Yordani, lakini mashujaa wenu wote, wakiwa wamevikwa silaha kikamilifu lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu hadi 15BWANA awape nao raha, kama alivyokwisha kufanya kwa ajili yenu hadi wao nao watakapokuwa wamemiliki nchi ile BWANA Mungu wenu anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kukalia nchi yenu wenyewe, ambayo Mose mtumishi wa BWANA aliwapa mashariki ya Yordani kuelekea linakochomoza jua.”

16Ndipo wakamjibu Yoshua, “Cho chote ambacho umetuagiza tutafanya na po pote utakapotutuma tutakwenda. 17Kama vile tulivyomtii Mose kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. BWANA Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Mose. 18Ye yote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au cho chote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”

Copyright information for Neno