Joshua 6

Yeriko Yatekwa Na Kuangamizwa

1Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa ajili ya Waisraeli. Hakuna mtu ye yote aliyetoka au kuingia.

2Kisha BWANA akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na watu wake wa vita. 3Zunguka mji mara moja pamoja na watu wako wote wa vita. Fanya hivi kwa siku sita. 4Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo waume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. 5Utakaposikia makuhani wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na watu watakwea, kila mtu aingie ndani moja kwa moja kutokea pale alipo.”

6Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la BWANA na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo waume mbele yake.” 7Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkazunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la BWANA.”

8Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba wenye kuzibeba zile baragumu saba mbele za BWANA, wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la BWANA likawafuata. 9Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma waliokuwa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa. 10Bali Yoshua aliwaagiza watu, “Msipige kelele za vita, msipaze sauti zenu, wala kusema neno lo lote mpaka siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!” 11Basi akalipeleka Sanduku la BWANA kuzunguka huo mji, likazungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala.

12Yoshua akaamka mapema asubuhi iliyofuata na makuhani wakalichukua Sanduku la BWANA. 13Makuhani saba wakachukua zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la BWANA wakizipiga hizo baragumu. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao, walinzi waliokuwa nyuma wakalifuata Sanduku la BWANA, huku makuhani wakiendelea kuzipiga hizo baragumu. 14Siku ya pili wakazunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita.

15Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakazunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. 16Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipopiga baragumu kwa sauti kubwa, Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana BWANA amewapa mji huu! 17Mji huu pamoja na vyote vilivyomo ndani yake utawekwa wakfu kwa BWANA kwa kuangamizwa kabisa. Ila Rahabu tu, yaani yule kahaba na wote ambao wako pamoja naye nyumbani mwake ndio watakaosalimishwa, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. 18Lakini mjiepushe na vitu vilivyowekwa wakfu, msije mkachukua cho chote katika hivyo, msije mkajiletea maangamizi katika maskani ya Israeli na kuiletea taabu. 19Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa BWANA, lazima viletwe katika hazina.”

20Wakati baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele, kwa sauti ya baragumu, na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akasonga mbele moja kwa moja kutokea pale alipokuwa kutokea kila upande na kuuteka mji. 21Wakauweka mji wakfu kwa BWANA, na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee, ng'ombe, kondoo na punda.

22Yoshua akawaambia wale watu wawili waliokuwa wameipeleleza nchi, “Nendeni nyumbani kwa yule kahaba, mleteni pamoja na wote waliomo nyumbani mwake, kulingana na kiapo chenu kwake.” 23Basi wale watu waliofanya upelelezi wakaenda kumleta Rahabu, baba yake na mama yake, ndugu zake na watu wote waliokuwa pamoja naye nyumbani mwake. Akaleta jamaa yake yote na kuwaweka mahali nje karibu na kambi ya Israeli.

24Kisha wakauchoma mji wote na kila kitu kilichokuwamo ndani yake. Lakini fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na chuma wakaviweka katika hazina ya nyumba ya BWANA. 25Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu yule kahaba, jamaa yake yote na wote waliokuwa wa kwake, kwa sababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko, naye anaishi miongoni mwa Waisraeli hata leo.

26Wakati ule Yoshua akatamka kiapo hiki akasema, “Alaaniwe mbele za BWANA mtu atakayeinuka kuujenga tena mji huu wa Yeriko: “Kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza wa kiume
ataweka misingi yake;
kwa gharama ya mtoto wake wa mwisho
ataweka malango yake.”27Hivyo BWANA alikuwa pamoja na Yoshua, na sifa zake zikaenea katika nchi ile yote.

Copyright information for Neno