Judges 18

Wadani Wahamia Laishi

1 aKatika siku hizo Israeli walikuwa hawana mfalme.

Katika siku hizo kabila la Wadani walikuwa wanatafuta mahali pao wenyewe pa kuishi, kwa sababu walikuwa hawajafika kwenye urithi wao miongoni mwa makabila ya Israeli.
2 bHivyo Wadani wakatuma mashujaa watano kutoka Sora na Eshtaoli ili kupeleleza nchi na kuichunguza. Hawa watu waliwakilisha koo zao zote. Waliwaambia, “Nendeni mkaichunguze hiyo nchi.”

Watu hao wakaingia katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao wakafika nyumba ya Mika, ambako walilala usiku huo.
3 cWalipofika karibu na nyumba ya Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi; hivyo wakaingia humo na kumuuliza, “Ni nani aliyekuleta hapa? Unafanya nini mahali hapa? Kwa nini uko hapa?”

4 dAkawaeleza yale Mika aliyomtendea, naye akasema, “Ameniajiri nami ni kuhani wake.”

5 eKisha wakamwambia, “Tafadhali tuulizie kwa Mungu kama safari yetu itafanikiwa.”

6 fYule kuhani akawajibu, “Enendeni kwa amani. Safari yenu ina kibali cha Bwana.”

7 gBasi hao watu watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa utulivu na bila mashaka. Nchi yao haikupungukiwa na kitu chochote, hivyo wakawa tajiri. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote.

8Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?”

9 hWakajibu, “Twendeni, tukapigane nao! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki. 10 iMtakapokwenda huko mtakuta watu waliotulia walio salama, nayo nchi hiyo ni kubwa na Mungu ameitia mikononi mwenu, nayo ni nchi ambayo haikupungukiwa na kitu chochote kilicho duniani.”

11 jNdipo watu 600 toka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli. 12 kWalipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Dani
Mahane-Dani maana yake Kambi ya Dani.
mpaka leo.
13 mKutoka hapo wakaendelea mbele mpaka nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika.

14 nNdipo wale watu watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mwajua kuwa mojawapo ya nyumba hizi kuna naivera, sanamu ndogo za nyumbani, sanamu ya kuchonga na sanamu ya kusubu? Sasa basi fikirini mtakalofanya.” 15Basi wakaingia humo na kwenda kwenye nyumba ya yule kijana Mlawi katika nyumba ya Mika na kumsalimu. 16Wale Wadani 600, waliovaa silaha za vita, wakasimama penye ingilio la lango. 17 oWale watu watano waliokwenda kupeleleza nchi wakaingia ndani na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani pamoja na ile sanamu ya kusubu, wakati yule kuhani akiwa amesimama pale penye ingilio la lango pamoja na wale watu 600 waliokuwa wamejifunga silaha za vita.

18 pHao watu walipoingia katika nyumba ya Mika na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, pamoja na ile sanamu ya kusubu, yule kuhani akawauliza, “Mnafanya nini?”

19 qWakamjibu, “Nyamaza kimya! Weka mkono wako juu ya kinywa chako na ufuatane nasi, uwe baba yetu na kuhani wetu. Si ni afadhali utumikie kabila na ukoo katika Israeli kama kuhani kuliko kumtumikia mtu mmoja na watu wa nyumbani mwake?” 20Yule kuhani akafurahi. Akachukua ile naivera, zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, na sanamu ya kuchonga, naye akaenda pamoja na wale watu. 21Ndipo wakageuka na kuondoka wakiwatanguliza mbele watoto wao wadogo, wanyama wao wa kufugwa na mali zao.

22Walipokuwa wamesafiri umbali kidogo toka nyumbani kwa Mika, watu walioishi karibu na Mika wakaitwa wakakusanyika pamoja, nao wakawafikia Wadani. 23Walipofuatilia wakipiga kelele Wadani wakawageukia na kumwambia Mika, “Una nini wewe hata ukaja na kundi la watu namna hii ili kupigana?”

24Akawajibu, “Mmechukua miungu yote niliyoitengeneza, mkachukua na kuhani wangu, nanyi mkaondoka. Nimebaki na nini kingine? Mnawezaje kuniuliza, ‘Una nini wewe?’ ”

25Wadani wakamjibu, “Usibishane na sisi, la sivyo watu wenye hasira kali watakushambulia, nawe na watu wa nyumbani mwako mtapoteza maisha.” 26 rBasi Wadani wakaenda zao, naye Mika alipoona kuwa wana nguvu kumliko yeye, akageuka na kurudi nyumbani kwake.

27 sKisha wakachukua vile Mika alivyokuwa ametengeneza, na kuhani wake, wakaendelea hadi Laishi, dhidi ya watu walio na amani, wasiokuwa na wasiwasi. Wakawashambulia kwa upanga na kuuteketeza mji wao kwa moto. 28Hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa, kwa kuwa kulikuwa mbali sana na Sidoni na hawakuwa na ushirikiano na mtu mwingine yeyote. Mji ulikuwa kwenye bonde karibu na Beth-Rehobu.

Wadani wakaujenga upya huo mji na kuishi humo.
29Wakauita ule mji Dani kwa kufuata jina la baba yao aliyezaliwa na Israeli, ingawa mji huo ulikuwa ukiitwa Laishi hapo kwanza. 30 tKisha Wadani wakajisimamishia sanamu ile ya kuchonga, naye Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Mose pamoja na wanawe walikuwa makuhani wa kabila la Wadani mpaka nchi hiyo ilipotekwa. 31 uWakaisimamisha na kuiabudu hiyo sanamu ya kuchonga ya Mika aliyokuwa ameitengeneza, wakati wote ule nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Shilo.

Copyright information for SwhNEN